BUNGE limeelezwa kuwa hali mbaya inayolikabili Shirika la Umeme (Tanesco)
imefanya shirika hilo kusimamisha huduma yake ya kuwaunganishia wateja
wapya umeme.
Lengo la Serikali ni kufikia walau asilimia 30 ya kaya za Watanzania wanaotumia umeme
ifikapo mwaka 2015 na ili kufikia lengo hilo, ilikadiriwa kuwa ni
lazima Tanesco iunganishe wateja wapatao 137,000 kwa mwezi kuanzia Machi
2012.
“Kutokana na hali mbaya ya kifedha na kiuendeshaji wa shirika, lengo hili halitaweza kufikiwa
kwani Tanesco inashindwa kulipia vifaa vya kutosha kwa wakati,”
alisema Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini,
January Makamba.
Alisema shirika kwa sasa linaelemewa na mzigo mkubwa na hali hiyo ikiendelea, litashindwa
kutimiza majukumu yake na akataka hali hiyo irekebishwe haraka kwani ipo hatari nchi kuingia
kwenye mgawo mkubwa wa umeme wakati wowote wa kiangazi.
Alisema pia kuwa kutokana na shirika hilo kuwa katika hali mbaya ya
kifedha, wagavi wake wanatishia kusimamisha huduma mbalimbali kwa
shirika hilo.
Pia Tanesco imeshindwa kupata fedha za kukarabati miundombinu ya
usafirishaji na usambazaji wa umeme hali inayofanya kuongezeka kwa uhaba
wa umeme.
Bunge pia liliambiwa na mwenyekiti huyo kuwa mpango wa dharura ulioahidiwa na Serikali
haujatekelezwa kwa kiasi na kiwango kama ilivyoahidiwa bungeni mwaka jana.
Makamba alisema katika megawati 572 zilizoahidiwa kuzalishwa kati ya
Agosti 2011 hadi Desemba 2011 ni megawati 342 tu ndizo zimezalishwa.
Kutokana na hatari hiyo ya nchi kuingia gizani wakati wowote, Kamati
hiyo ya Bunge imeishauri Serikali kutoa dhamana yake ili shirika hilo
liweze kukopa fedha kiasi cha Sh bilioni 408 ili ilipie madeni yake.
Kwa upande wake, Kamati ya Fedha na Uchumi katika taarifa yake
ilisema Tanesco inadaiwa Sh bilioni 105 na kampuni za kufua umeme wa
dharura na Sh bilioni 164 zinadaiwa na wadeni wengine; hivyo kufanya
hadi kufikia Machi mwaka huu, shirika hilo lilikuwa linadaiwa jumla ya
Sh bilioni 269.
Lakini pia kamati hiyo imeonya kuwa kiasi cha Sh bilioni 408
zitakazochukuliwa na shirika hilo kama mkopo kutoka benki za ndani,
gharama kubwa ya mkopo huo pamoja na ulipaji wa riba utafanya gharama za
uzalishaji kuwa za juu kwa matumizi ya Tanzania.
“Malipo haya yanaongeza matumizi ya Serikali yenye ukusanyaji mdogo wa mapato,” alisema
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Fedha na Uchumi, Dk. Abdallah Kigoda.
Dk. Kigoda alisema mpango wa Serikali wa kuongeza umeme hautaleta tija ikiwa Gridi ya Taifa itaendelea kama ilivyo sasa.
Kwa upande wake, Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Mashirika ya Umma ni
moja ya shirika linalotumia fedha za umma vibaya kinyume cha Sheria ya
Manunuzi ya Umma.
Kamati hiyo imetoa mfano wa Tanesco kutumia Sh bilioni 1.8 kukarabati gati mojawapo katika
Bwawa la Mtera wakati bajeti ya ukarabati wa bwawa hilo ulikuwa ni Sh milioni 65.
Kamati hiyo pia imelishutumu shirika hilo kwa kushindwa kukusanya
maduhuli kwani hadi kufikia Desemba mwaka 2010, Tanesco ilikuwa inawadai
wateja wake Sh bilioni 245 na kati ya fedha hizo, Sh bilioni 15
zinadaiwa taasisi za serikali.
No comments:
Post a Comment