Sunday, April 22, 2012

Nundu asigana na Naibu wake

WAZIRI wa Uchukuzi, Omar Nundu amesema anapigwa vita na Naibu Waziri wake, Athumani
Mfutakamba baada ya yeye kupinga Kampuni ya CCCC kupewa zabuni ya kupanua Bandari ya Dar es Salaam.

Akizungumza jana na waandishi wa habari mjini hapa, Nundu alisema CCCC iliwahi kwenda kumshawishi yeye ili akazungukie katika nchi mbalimbali kutembelea miradi ya kampuni hiyo, lakini alikataa kwa vile alijua kuwa kufanya hivyo ni kama hongo.

Nundu alisema lakini cha ajabu, Naibu Waziri wake alipofuatwa na kampuni hiyo, alikubali na akapelekwa kwenye nchi za Mauritius, China na Guinea Bissau bila hata kumtaarifu bosi wake.

Alisema uhusiano wake na Naibu Waziri ulianza kuingia dosari wakati wa ujenzi la jengo la maegesho katika Bandari ya Dar es Salaam ambalo Nundu aliusimamisha baada ya kuona zabuni ya ujenzi wake hauna mashiko.

Aidha, Nundu alidai Mfutakamba aliwahi kumsemea yeye kwa Rais Jakaya Kikwete wakati alipotembelea Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA) kuwa anazuia mradi huo.

“Nashukuru Mungu Rais alikuwa ameshapata taarifa ubabaishaji uliopo kwenye mradi
huo naye akaomba ujenzi wake usitishwe kwanza,” alisema Waziri huyo.

Alisema amekuwa mstari wa mbele kupinga miradi yote yenye dalili za rushwa, lakini baadhi ya watendaji ndani ya taasisi zilizoko chini ya wizara yake, wanamshutumu kuwa anaingilia maslahi ya mashirika hayo.

“Mimi ni kama mtu yuko porini na amevamiwa na majambazi anapiga kelele, lakini hakuna mtu wa kumsaidia,” alisema Nundu akimaanisha kuwa wanaompiga vita ni wale ambao wanataka kufuja fedha kwa kutumia miradi ambayo yeye anaona kuna mianya ya rushwa.

Kutokana na hali hiyo, Nundu asisitiza kuwa haoni sababu ya yeye kujiuzulu kwa kuwa hana kosa lolote alilolifanya na jambo analolitetea ni kwa maslahi ya nchi yake.

Alisema hana njaa ya kuiba fedha za umma, kwani kwa nafasi ambazo amewahi kushika tangu awe mtumishi sehemu mbalimbali nchini na nje ya nchi, ana fedha za kutosha za kuishi vizuri yeye na familia yake.

Alisema ana machungu na taifa lake na anafanya kazi ya uwaziri kama kulipa fadhila kwa taifa ambalo lilimsomesha ndio maana anapigwa vita kila kona, kwa sababu amebana ulaji wa baadhi ya watu ndani ya wizara yake na ndani ya TPA.

Nundu alisema sio kwamba yuko kwenye nafasi ya uwaziri kwa ajili ya kusaka fedha, bali anataka kulisaidia taifa lake na amekuwa anajitahidi kufanya kazi kwa maadili makubwa.

Mbunge huyo wa Tanga Mjini, ni miongoni mawaziri ambao inadaiwa ameshinikizwa ajiuzulu kutokana na wizara yake kufanya madudu, likiwemo suala la kuingilia utendaji wa Menejimenti ya TPA.

Lakini Nundu katika maelezo yake ya jana, alisisitiza kuwa hakuwahi kuingilia utendaji wa TPA,
bali anachotaka yeye ni ujenzi wa gati namba 13 na 14 upate mwekezaji ambaye amefuata taratibu na gharama zake ziwe zimehakikiwa na Serikali.

Alisema kitendo cha Menejimenti ya TPA kumtafuta mwekezaji bila kushindanishwa ni ukiukwaji wa taratibu za Serikali.

Alisema kuna kampuni zipatazo 12 ziko tayari kujenga gati hiyo. Alisema anataka kila kampuni ipewe fursa ya kufanya upembuzi yakinifu waone ni kampuni gani yenye gharama nafuu.

Kwa upande wake, Mfutakamba alipoulizwa kuhusu madai ya bosi wake, alisema safari alizosafiri kwenda nchini China, Guinea na Mauritius aliondoka wakati waziri huyo akiwa safari ndio maana hakumwaga.

Lakini alisema alifuata taratibu zote za kiserikali kwani alimwaga Waziri Mkuu na akapewa ruhusa.

Alisema nia yake ya kwenda kutembelea miradi ya kampuni ya CCCC ni kutaka kuona uwezo wa kampuni hiyo badala ya kuwapa mradi huo wa ujenzi wa upanuzi wa bandari bila kujiridhisha.

“Kweli nilienda China ambako niliona wanajenga reli, wanaongeza kina cha bahari na wanajenga magati katika miradi yao hiyo,” alisema naibu waziri huyo na kukanusha kuondoka bila kumwaga bosi wake huyo kuwa hawezi kufanya hivyo kwa kuwa anafahamu taratibu za
kazi.

Alisisitiza kuwa baada ya kurudi nchini, aliandika ripoti nzuri na kuiwasilisha kwa bosi wake na kwa Waziri Mkuu kuhusu alichokiona kwa wawekezaji wa CCCC ambao wameomba kupanua bandari ya Dar es Salaam.

Alisema katika miradi yote inayotekelezwa na taasisi zilizo chini ya wizara hiyo, amekuwa anamshauri bosi wake kwa maandishi njia nzuri ya kushughulikia miradi hiyo na kufanya hivyo sio kwamba anampiga vita.

“Mimi ndiye mshauri wake mkuu nilichomweleza kuhusu TPA niliweka wazi kuwa lile ni shirika
linaloruhusiwa kisheria kufanya manunuzi yake,” alisema na kuongeza kuwa alimshauri vile kwa kutambua kuwa TPA ina Bodi ambayo inajua namna nzuri ya kuwapata wawekezaji kuliko wizara ikiingilia.

Alisema alimshauri pia kuwa kazi ya wizara ni kuandaa sera, miongozo na taratibu za namna ya kumpata mwekezaji.

“Nimekuwa mkuu wa wilaya kwa miaka mitano, nafahamu taratibu za kiserikali za kuondoka nje ya nchi na majukumu ya wizara,” alisema Mfutakamba ambaye kabla ya kuwania ubunge na kushinda Jimbo la Igalula mkoani Tabora, alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Kilolo mkoani
Iringa.

Akizungumzia juu ya ushauri alioutoa kuhusu upanuzi wa TPA, Mfutakamba alisoma barua aliyoiandika alishauri iwepo mipaka ya kimajukumu kati ya TPA na wizara katika utekelezaji wa mradi huo wa ujenzi wa gati namba 13 na 14.

Alisema alifafanua pia kuwa jukumu la kumlipa mwekezaji ni la TPA hivyo ni vyema mamlaka hiyo kupitia Bodi yake ikaweka vigezo wanavyoona vinafaa katika kumpata mwekezaji na lengo ni kumpatia mwekezaji ambaye atalipa taifa faida.

“Hayo ndio naweza kusema, maana nafahamu kushauri sio kumpiga vita mtu,” alisema naibu
waziri huyo na kuongeza kuwa ni vyema sasa kile ambacho kimeazimiwa na Bunge kiachwe kifanye kazi kwa Serikali kujiridhisha katika kufanya tathmini ya gharama halisi za ujenzi wa mradi huo.

Kampuni ya CCCC katika upembuzi yakinifu ilioufanya imebainisha gharama za ujenzi wa gati hilo kuwa ni Dola za Marekani milioni 540, lakini Nundu anadai kuwa kati ya kampuni 12, kampuni mbili zimekubali kujenga gati hilo kwa Dola za Marekani milioni 300.

No comments:

Post a Comment