Monday, April 23, 2012

Spika aitupa ripoti ya Jairo

Aeleza ugumu wa utekelezaji wa kanuni ya 94

SPIKA wa Bunge, Anne Makinda, amesema hajaridishwa na majibu ya serikali kuhusu taarifa ya utekelezaji wa maazimio ya kamati ya Bunge kuhusu sakata la aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, David Jairo, hivyo kuirudisha serikalini.

Spika Makinda alitoa kauli hiyo jana, baada ya Mbunge wa Karatu, Mchungaji Israel Natse, kutaka mwongozo wa Spika katika suala hilo kutojadiliwa huku mkutano wa Bunge ukiwa unaahirishwa.

“Mheshimiwa Spika naomba kupata mwongozo wako katika order paper inaonekana Bunge linaahirishwa leo, lakini hakuna taarifa ya serikali kuhusu utekekezaji wa maazimio ya kamati ya Bunge kuhusu suala la Jairo na mpaka sasa hatujaambiwa chochote,” alisema.

Akijibu Spika Makinda alisema, “Tulikuwa tuweke katika mkutano huu, lakini mimi nimeyakataa majibu kwa kuwa sijaridhishwa, hivyo nimerudisha serikalini,” alisema Spika.
Jairo, alisimamishwa kazi kutokana na sakata la kuzichangisha fedha taasisi zilizokuwa chini ya wizara hiyo kwa lengo la kufanikisha kupitisha bajeti bungeni.

Kutokana na hali hiyo, Bunge liliunda Kamati Teule ya Bunge iliyoongozwa na Mbunge wa Tunduru Kaskazini, Ramo Makani, kuchunguza uhalali wa utaratibu wa wizara hiyo kuchangisha fedha hizo na kubaini kasoro kadhaa kabla ya kutoa mapendekezo yake.

Kamati hiyo iliundwa baada ya kuibuka mvutano baina ya mihimili miwili ya dola, Bunge na Serikali baada ya aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo, kutangaza hadharani kumrejesha kazini Jairo aliyekuwa amesimamishwa kazi kwa tuhuma hizo zilizotolewa bungeni dhidi yake.

Hata hivyo, siku chache baada ya wabunge kuja juu kupinga uamuzi huo wa Luhanjo, Ikulu ilitangaza rasmi kushughulikia tuhuma za rushwa zinazomkabili Jairo, baada ya Rais kumpa likizo yenye malipo na alipofanya uteuzi wa makatibu wakuu alimwacha pembeni na nafasi hiyo akampa Eliakimu Maswi.

Wakati huohuo, Spika wa Bunge alisema leo wabunge wamelazimika kujadili kamati ya mipango baada ya kuahirishwa kwa Bunge kutokana na kubanwa na kanuni ya 94.
Alisema kutokana na hali hiyo, kuna haja ya kuiangalia upya kanuni hiyo, hivyo mjadala wa kamati hiyo utafanyika katika ukumbi wa Msekwa.

“Kanuni ya 94 imekuwa na ugumu katika utekelezaji, hivyo kamati ya uongozi imeamua mjadala wa mpango wa maendeleo ya taifa kwa mwaka 20012/2013 ufanyike kesho (leo) katika ukumbi wa Msekwa, ili Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na maofisa wengine waweze kushiriki katika mjadala huo na kutoa majibu kwa hoja zitakazoibuliwa na wabunge,” alisema.

No comments:

Post a Comment