Monday, April 23, 2012

CHADEMA yaishukia Ikulu

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimeishambulia Ofisi ya Rais Ikulu juu ya kauli yake kwamba Rais Jakaya Kikwete alikuwa hajakutana na Waziri Mkuu Mizengo Pinda kumjulisha kile kilichotokea bungeni wiki jana, kinadhihirisha ombwe kubwa la uongozi katika ofisi ya Rais na udhaifu wa kiuongozi wa Rais na serikali kwa ujumla.

Taarifa ya CHADEMA iliyotolewa na Mkurugenzi wa Habari na Uenezi, John Mnyika, ilisema kuwa Ikulu imeonyesha bayana kuwa Rais Kikwete ni mzito wa kuchukua hatua kwa kuwa masuala ambayo yamezuka bungeni anayafahamu kwa kuwa yamepitia kwenye Baraza la Mawaziri ambalo yeye analiongoza na pia yapo kwenye taarifa mbalimbali ambazo mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali amemkabidhi nakala kwa nyakati mbalimbali.

Aidha CHADEMA imesema taarifa hiyo ya Ikulu imedhihirisha namna ambavyo safari za mara kwa mara za Rais zinavyolifanya taifa likose uongozi wake katika masuala ya msingi yanayoikabili nchi; hivyo ni muhimu asitishe safari ili kupunguza matumizi ya fedha wakati huu ambapo serikali ina ufisadi na matumizi makubwa hatua ambayo itamwezesha kubaki nchini kushughulikia masuala muhimu yanayolikabili taifa.

Kwa upande mwingine, CHADEMA imesema taarifa hiyo ya Ikulu iliyokuwa ikikanusha habari zilizoandikwa na Tanzania Daima juzi, inadhihirisha kwamba hakuna mawasiliano ya karibu na ya mara kwa baina ya Rais Kikwete na Waziri Mkuu Pinda wakati kwa mujibu wa ibara ya 52(3) na 53 (1) Waziri Mkuu ndiye msimamizi wa utekelezaji wa maagizo ya Rais anayewajibika kwa Rais.
“Hali hii imekuwa ikijirudiarudia katika matukio kadhaa kwenye kipindi cha kati ya mwaka 2008 mpaka 2011; ikiwemo matukio ya kashfa ya aliyekuwa Katibu Mkuu wa Nishati na Madini, David Jairo.

“Baraza hili la mawaziri kuendelea mpaka sasa kwa hali hii ni ishara ya udhaifu wa mamlaka ya uteuzi ambayo ni Rais Kikwete kwa kuwa ibara ya 57 (1) (c) ya Katiba imempa madaraka kufuta uteuzi na kuwaondoa madarakani mawaziri; hivyo Rais Kikwete athibitishe kwa matendo badala ya maneno matupu kuwa hawalindi mawaziri kwa kuwafukuza waliotajwa kwa kukiuka sheria,” ilisema taarifa ya CHADEMA.

Juzi Ikulu ilikanusha habari kuwa Rais alikuwa amewasiliana na Waziri Mkuu Pinda kuhusiana na suala la kujiuzulu kwa mawaziri, ikidai kuwa tangu awasili kutoka Brazil, Kikwete alikuwa hajakutana wala kuzungumzia suala hilo na waziri wake.

No comments:

Post a Comment