MALALAMIKO ya aliyekuwa Katibu Mkuu wa CCM, Philip Mangula dhidi ya
Mbunge wa Kawe, Halima Mdee (Chadema) na shauri linalomhusu Meya wa Jiji
la Dar es Salaam, Didas Masaburi anayetuhumiwa kuwatukana wabunge kuwa
wanafikiri kwa kutumia makalio, yamemalizika kusikilizwa na Kamati ya
Bunge.
Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge katika taarifa yake ya
utekelezaji kwa mwaka 2011/12 iliyowekwa mezani mwishoni mwa wiki katika
Mkutano wa Saba wa Bunge unaoendelea mjini hapa, inaeleza kuwa kamati
imemaliza kusikiliza mashauri hayo na uamuzi wameupeleka kwa Spika Anne
Makinda.
Mangula anamlalamikia Mdee kuwa wakati akiwasilisha hotuba ya
Msemaji wa Kambi ya Upinzani kwenye bajeti ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya Makazi katika mwaka huu wa fedha, alitoa kauli
iliyomhusisha kuwa anamiliki hekta 2,000 za ardhi katika Kijiji cha
Wami-Dakawa wilayani Mvomero.
Baada ya kauli hiyo, Mangula aliibuka kwenye vyombo vya habari na
kukanusha madai hayo ya Mdee na akamtaka athibitishe kauli yake.
Suala hilo liliwasilishwa mbele ya kamati kwa mujibu wa Kanuni za
Kudumu za Bunge ambayo inatoa haki ya raia kujitetea na kusafisha dhidi
ya kauli zinazotolewa bungeni.
“Kamati ilishughulikia suala hili hatua zake zote na taarifa ya kamati ikawasilishwa kwa spika kwa hatua zaidi,” ilieleza.
Kuhusu suala la Masaburi, liliwasilishwa baada ya Mbunge wa
Kinondoni, Idd Azzan kuomba mwongozo wa Spika kuhusu kauli ya Meya huyo
wa Dar es Salaam inayowadhalilisha wabunge na Spika akaamua kuamuru
suala hilo lishughulikiwe na Kamati hiyo.
Taarifa hiyo iliyotiwa saini na mwenyekiti wake Hassan Ngwilizi, pia
ilieleza suala hilo limemalizika kusikilizwa. Shauri la tatu ambalo
lilifikishwa mbele ya kamati hiyo lilifikishwa na
Masaburi mwenyewe dhidi ya kauli zilizotolewa bungeni dhidi yake na baadhi ya wabunge.
Wabunge hao ni Godfrey Zambi ambaye ni Mbunge wa Mbozi Mashariki (CCM), Mdee na
Mbunge wa Mafia, Abdulkarim Shah (CCM).
Masaburi alilalamikia kauli za wabunge hao walizozitoa wakati
wakichangia hotuba ya Wizara ya Uchukuzi kwa mwaka huu wa fedha ambapo
walimhusisha na uuzwaji wa Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA).
No comments:
Post a Comment