Monday, April 30, 2012

Auawa kwa risasi akivamia shamba

WILAYA ya Arumeru imeendelea kukumbwa na matukio ya vifo baada ya mwananchi mmoja mwenye miaka kati ya 25 na 30, ambaye jina lake halijafahamika, kuuawa kwa kupigwa risasi na walinzi wa shamba la Mitomiwili lililoko Kilala, kata ya Sing’isi, Tengeru.

Mauaji hayo yametokea ikiwa ni siku moja baada ya kuuawa kwa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kata ya Usa River, Msafiri Mbwambo.

Mpaka sasa idadi ya watu waliokufa kwa kipindi cha wiki moja katika matukio ya kutatanisha ni sita baada ya vijana wengine wanne kukutwa wamekufa na miili yao kutupwa kwenye maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Thobias Andengenye, alisema kuwa tukio hilo lilitokea juzi saa nne usiku wakati marehemu akiwa na kundi la wananchi wengine wanaokadiriwa kuwa kati ya 40 na 50 ambao walivamia shamba hilo la mwekezaji.

Alisema kuwa mwananchi mwingine ambaye pia jina lake halikupatikana mara moja alijeruhiwa vibaya na anapatiwa matibabu chini ya ulinzi wa polisi.

Kamanda huyo alifafanua kuwa walinzi hao wa shamba hilo ambao hakuwataja kwa majina walimuua marehemu huyo kwa kutumia bunduki aina ya shortgun wakati wa kulinda mali za tajiri yao.

Andengenye aliongeza kuwa wananchi hao baada ya kuvamia shamba hilo linalomilikiwa na kampuni ya Pulse and Agrocommodities, waliharibu mali kwa kuchoma matrekta manne, kuiba mifuko ya mbolea 300 huku wakivunja vioo vya gari lililokuwa limeegeshwa eneo hilo ambapo thamani halisi ya mali zilizoharibiwa bado haijajulikana.

Hata hivyo alisema kuwa mpaka sasa hakuna mtu anayeshikiliwa na polisi kuhusiana na matukio hayo licha ya jeshi hilo kuendelea na uchunguzi.

No comments:

Post a Comment