Sunday, April 22, 2012

RAIS KIKWETE AOMBOLEZA KIFO CHA BRIGEDIA JENERALI MWAKANJUKI


Rais Jakaya Mrisho Kikwete amemtumia salamu za rambirambi Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Dk. Ali Mohamed Shein kufuatia kifo cha mwanasiasa mkongwe Brigedia Jenerali Mstaafu Adam Mwakanjuki aliyefariki dunia katika Hospitali Kuu ya Jeshi, Lugalo jijini Dar-es-Salaam jana tarehe 19 April, 2012.

Marehemu amewahi kushika nafasi mbalimbali za uongozi visiwani Zanzibar zikiwemo za Uwaziri katika Wizara mbalimbali na pia kuwahi kuwa Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi.
"Pokea rambirambi zangu za dhati kwa kuondokewa na mzee wetu, kiongozi shupavu na mwanamapinduzi imara, ni pengo kubwa kwetu kwani Marehemu amekuwa mshauri wetu mkweli na muwazi, upendo na ucheshi wake pia ilikuwa faraja kwetu wakati wa vipindi vigumu na vyepesi" Rais ameeleza,

"Tutaukosa ushauri wake, upendo wake na mchango wake katika kila hali" Rais amesema na kumuomba Rais Dk. Ali Mohamed Shein kufikisha salamu zake za rambirambi kwa familia, wananchi wote na viongozi wenzake ambao marehemu amefanya nao kazi katika idara zote serikalini, jeshini, na pia katika Baraza la Wawakilishi.


Rais Jakaya Kikwete akitoa heshima za mwisho kwa Marehemu Brigedia Jenerali Mstaafu Adam Mwakanjuki mapema asubuhi leo Aprili 22, 2012 katika kambi ya JWTZ ya Kikosi cha Anga kabla ya kupelekwa Zanzibar kwa mazishi.…


Rais Jakaya Kikwete akitoa heshima za mwisho kwa Marehemu Brigedia Jenerali Mstaafu Adam Mwakanjuki mapema asubuhi leo Aprili 22, 2012 katika kambi ya JWTZ ya Kikosi cha Anga kabla ya kupelekwa Zanzibar kwa mazishi.
Rais Jakaya Mrisho Kikwete, Mkuu wa Majeshi Jenerali Davies Mwamunyange na Mhe. Aboud wakiangalia wakati jeneza lenye mwili wa Marehemu Brigedia Jenerali Mstaafu Adam Mwakanjuki ulipokuwa unaingizwa katika ndege mapema asubuhi leo Aprili 22, 2012 katika kambi ya JWTZ ya Kikosi cha Anga kabla ya kupelekwa Zanzibar kwa mazishi.
PICHA NA IKULU

Marehemu Mwakanjuki alianza siasa kabla ya Mapinduzi ya Zanzibar ya Januari 12, 1964 akianzia katika Chama Cha Afro Shiraz (ASP) na baadae Chama cha Mapinduzi.
"hatuna budi kumshukuru mwenyezi Mungu kwa mchango wa marehemu wakati wa uhai wake nasi twamuombea mapumziko mema ya milele, Amina" Rais amemuombea Dua na kuiomba familia ya marehemu kuwa na subira wakati huu wakuondokewa na mpendwa wao.

No comments:

Post a Comment