-Asema hakuna tatizo la Ardhi
-Waraka kumpinga Sioi wasambazwa
NAIBU
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Goodlucky Ole Medeye
amewatetea walowezi wanaomiliki maeneo makubwa ya ardhi katika Jimbo la
Arumeru Mashariki kwamba wanamiliki mashamba hayo kwa mujibu wa sheria.
Kauli
ya Ole Medeye ambaye alikuwa akimnadi mgombea wa CCM, Sioi Sumari
katika kampeni za uchaguzi mdogo wa jimbo hilo inapingana na ile
iliyotolewa na Rais Mstaafu, Benjamin Mkapa alipokuwa akizindua kampeni
za CCM, Machi 12 mwaka huu mjini Usa River.
Kadhalika, kauli hiyo
inapingana na kauli zote za makada wa CCM na vyama vya upinzani akiwamo
mgombea wa CCM Sioi ambao wanakiri kuwapo kwa matatizo makubwa ya ardhi
Arumeru, huku wakiahidi kuyashughulikia.
Mkapa akizungumzia matatizo
ya ardhi siku ya uzinduzi huo, kwanza alikanusha kuwa na ubia na
walowezi hao lakini akakiri kuwapo kwa matatizo hayo huku akiahidi
kwamba atafikisha suala hilo kwa Rais Jakaya Kikwete ili alipatie
utatuzi.
Mkapa alikiri kupokea taarifa za kuwapo kwa migogoro
mikubwa ya ardhi inayosababishwa na baadhi ya wawekezaji kuhodhi maeneo
makubwa na kusema kwamba kero hiyo iko katika hatua mbalimbali za
utatuzi wake.
“Yapo matatizo kadha wa kadha, wapo wawekezaji
ambao wamehodhi maeneo makubwa wakati hawayatumii, wapo ambao wamechukua
maeneo na kubadilisha matumizi yake na wapo ambao wamekiuka sheria za
uendeshaji wa maeneo waliyopewa,” alisema Mkapa.
Alisema suala
hilo atalifikisha kwa Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete na
kumshauri achukue hatua kwa kuwawajibisha watendaji wa serikali ambao
wameshindwa kuwajibika na kuchukua hatua za kisheria kwa wawekezaji
waliokiuka masharti.
Lakini jana, Ole Medeye alisema mashamba yote
13 yanayotajwa yanamilikiwa kihalali na kwamba ikiwa kuna tatizo lolote
basi wizara yake itafuatilia ili kuchukua hatua.
“Masuala ya
umiliki wa ardhi yanasimamiwa na sheria za nchi, kwa hiyo wawekezaji
hawa wanaotajwa, wanamiliki maeneo yao kwa mujibu wa sheria. Sasa kama
kuna maeneo hayajaendelezwa basi hilo ni suala la kuona jinsi ya
kuchukua hatua,” alisema Medeye katika mkutano wa kumnadi Sioi
uliofanyika katika Kijiji cha Sing’isi.
Medeye ambaye pia ni
Mbunge wa Arumeru Magharibi alisema Serikali imekuwa ikichukua hatua
madhubuti kutatua kero ya ardhi ndani ya wilaya hiyo na kwa sasa
itayatwaa mashamba yote yanayomilikiwa na watu binafsi endapo
hayataendelezwa ili yagawiwe kwa wananchi. Aliyataja mashamba ambayo
hayajaendelezwa kuwa ni Valeska, Madira na Tanzania Plantation.
Alisema
akiwa Naibu Waziri wa Ardhi tayari ametembelea mashamba yote na kwamba
Serikali inajipanga jinsi ya kutatua migogoro iliyopo. Alisema endapo
watamchagua mgombea wa CCM atashirikiana naye kwa kuwa atakuwa
anamkubusha juu ya utekelezaji wa kero za ardhi.
Alisema hoja za
wapinzani kwamba wanaweza kurejesha ardhi kwa wananchi si kweli kwani
ili kufikia hatua hiyo lazima sheria zifuatwe.
Amvaa Dk Slaa
Ole
Medeye alimshukia Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa kwamba
ameshindwa kutatua kero ya ardhi na maji katika Wilaya ya Karatu
alikokuwa mbunge kwa miaka 10 hivyo asirukie hoja ya Arumeru Mashariki.
Alisema
katika Wilaya ya Karatu inayoongozwa na Chadema, kuna mashamba 32
yanayomilikiwa na wawekezaji ambao kimeshindwa kuwanyang’anya.
Alisema
Karatu ambako Chadema kinashika dola kwa kuongoza halmashauri,
inaongoza kwa tuhuma za ufisadi kwa kuwa baadhi ya madiwani wa chama
hicho waligawana eneo la shule mojawapo ya msingi na kisha kujenga
vilabu vya pombe na nyumba za wageni karibu na shule hiyo.
Alisema
mmoja wa madiwani wa Chadema alibaini ufisadi huo na kuandika barua
wizarani kwake. Alisema alifunga safari kwenda Karatu ambako alishudia
madudu hayo na kisha kuvifuta viwanja hivyo.
Waraka wasambazwa
Watu
wasiojulikana jana walisambazwa waraka ambao unadaiwa kuandikwa na
wabunge wa CCM ambao wanapiga vita ufisadi wakitaka mgombea wa CCM, Sioi
Sumari asichaguliwe kwani atawaongezea nguvu mafisadi kuelekea Uchaguzi
Mkuu mwaka 2015.
Waraka huo ambao jana ulikuwa ukisambazwa katika
mitaa mbalimbali ya Usa River na kwenye mikutano ya kampeni ya Chadema
na CCM, una kichwa cha habari kisemacho “Chama cha Mapinduzi na Kamati
maalum dhidi ya ufisadi.”
Katika waraka huo ambao haujasainiwa na
mtu yeyote unadaiwa kutumwa kwa wananchi wa Meru na wabunge wa CCM ambao
picha zao zimeambatanishwa.
“Tunawaandikia waraka huu kwa kuwa
tunaamini kabisa kwa kufanya hivyo tunamfurahisha Mungu na kuwanusuru na
kiu ya damu ya baadhi ya viongozi wa nchi hii. Mafisadi hawa
wameshindwa kabisa kuacha ufisadi na sasa wanatumia fedha walizowaibia
Watanzania…” inasomeka sehemu ya barua hiyo.
Kadhalika waraka huo
unamtaja mmoja wa makada wakongwe wa CCM (jina tunalihifadhi) kwamba
ameamua kutunisha misuli yake na kuhakikisha Sioi anashinda ubunge
Arumeru, lengo likiwa ni kuonyesha kwamba ana nguvu zaidi kwa kutumia
fedha zake.
Chadema jana walikana kuufahamu waraka huo na kusema kuwa wenye uzoefu wa kuandika nyaraka za aina hiyo ni CCM.
Mkuu
wa operesheni wa uchaguzi huo wa Chadema, John Mrema alisema: “Sisi
hatuwezi kuandaa waraka kama huu, haya ni mambo ya CCM wenyewe.”
Meneja Kampeni wa CCM, Mwigulu Nchemba hakupatikana jana kuzungumzia waraka huo.
Chadema chadai kadi 668 Polisi
Chadema
jana kimeitaka Polisi kurejesha kadi za kupigia kura za watu 668 ambazo
zinashirikiliwa Kituo chake cha Usa River na Kituo Kikuu cha Arusha.
Mrema
alisema wamepata taarifa kutoka polisi za kuwapo vitambulisho vya
kupiga kura 206 katika Kituo cha Usa River ambavyo vimeachwa na watu
waliokwenda kuwawekea dhamana watuhumiwa. Alisema katika Kituo Kikuu
Arusha kuna kadi za vijana wa Meru 462 ambao wanafanyakazi za kubeba
mizigo ya watalii katika Mlima Meru maarufu kama Wapagazi.
Mkuu wa
Oparesheni ya Polisi katika uchaguzi wa Arumeru Mashariki, Isaya Mngulu
alisema asingeweza kutoa maelezo yoyote kuhusu madai hayo akisema
maofisa wa ngazi za juu wa polisi walikuwa kwenye kikao.
CCM wapigwa mawe
Jana,
msafara wa CCM ulishambuliwa kwa mawe katika Kijiji cha Sing’is
ulipokuwa umekwenda kwa ajili ya kumnadi mgombea wake, Sioi Sumari.
Katika
tukio hilo, mmoja wa vijana wanaoshukiwa kuhusika na shambilio hilo
alikamatwa na vijana wanaosadikiwa kuwa wa CCM na kupigwa hadi kupoteza
fahamu hadi alipookolewa na polisi waliokuwa nyuma ya msafara huo.
Tukio
hilo lilitokea saa 6.30 mchana jana wakati msafara huo wa CCM ulipofika
eneo la Chama na ghafla walijitokeza vijana watatu mbele ya magari hayo
kisha kuanza kuyashambulia kwa mawe. Vijana hao watatu walikuwa wamevaa
beji zenye picha ya mgombea wa Chadema, Joshua Nassari.
Katika
tukio jingine, kijana ambaye hakufahamika jina, juzi jioni alipigwa
kwenye mkutano wa CCM katika Viwanja vya Ngaresero baada ya kuishangilia
helkopta ya Chadema iliyopita kwenye eneo hilo wakati Sioi akihutubia.
Huko
Seela Sing’isi, vijana watatu ambao walikuwa wakinyoosha vidole viwili
ambayo ni alama ya Chadema, jana walikamatwa kwenye mkutano wa kumnadi
Sioi. Vijana hao walikuwa wamesimama nyuma ya eneo la mkutano na
walishikiliwa na polisi baada ya Ole Medeye kutamka kwamba wanaoiunga
mkono CCM wanyooshe mikono juu na wao wakanyoosha alama ya vidole
viwili.
No comments:
Post a Comment