Thursday, March 29, 2012

Shahidi akiri sheria ya uchaguzi ilikiukwa

SHAHIDI wa tano upande wa utetezi katika kesi ya uchaguzi mkuu wa ubunge katika  Jimbo la Segerea jijini Dar es Salaam, Protas Tarimo amekiri kuwa sheria ya uchaguzi ilikiukwa.
Shahidi huyo, Ofisa Mtendaji Mwandamizi Kata ya Vingunguti  ambaye alikuwa msimamizi msaidizi wa uchaguzi katika kata hiyo alikiri ukiukwaji huo wa sheria jana wakati akihojiwa na wakili wa upande wa madai.

Kesi namba 98 ya mwaka 2011 inayosikilizwa na Jaji Profesa Ibrahim Juma, ilifunguliwa na aliyekuwa mgombea wa kiti hicho kupitia Chadema, Fredy Mpendazoe ambaye anapinga matokeo yaliyompa ushindi mbunge wa sasa wa jimbo hilo Dk Makongoro Mahanga.

Akihojiwa na wakili wa Mpendazoe, Peter Kibatala shahidi huyo alisema wakati uchaguzi gari la mtu binafsi lilitumika katika shughuli za uchaguzi badala ya gari la Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) jambo ambalo alikiri ni kinyume cha sheria.


Alipoulizwa kuwa gari hilo lilikuwa ni la nani, alijibu kuwa hajui, lakini kwa mujibu wa ushahidi uliotolewa mahakamani hapo na upande wa madai, gari hilo lilikuwa ni la mgombea wa udiwani katika kata hiyo wa Chama Cha Mapinduzi(CCM), Asah Simba.

Shahidi wa nne upande wa madai Bazil Ng'oholope  katika ushahidi wake, alidai wakati wakielekea ofisi ya WEO, msimamizi wa uchaguzi wa Kata ya Vingunguti alipanda gari moja na mgombe wa CCM, Assa Simba na mawakala wake wakiwa na fomu za matokeo.

Shahidi huyo ambaye pia aliwakuwa mgombea wa udiwani katika kata  hiyo kupitia Chadema, aliongeza kuwa yeye na wagombea wengine walipanda gari lingine la mtu binafsi ambalo baadaye walighundua kuwa lilikuwa la mgombea huyo wa CCM.

"Baada ya kufika tulishuka na mimi nikawa ninazungumza na mgombea wa udiwani wa Chama cha Wananchi (CUF)  na walimuona Simba akiegesha vizuri gari tulilokuwa tumelipanda sisi.Niliingiwa na wasiwasi nilipogundua kuwa gari lile lilikuwa la mgombea mwenzetu,” alisema.

Lakini jana alipoulizwa na Wakili Kibatala kama gari la mgombea mmoja au mtu binafsi kuwabeba wagombea wengine na mawakala, ni sahihi kisheria,  shahidi huyo alijibu kuwa wakati wa uchaguzi sio sahihi gari binafsi kufanya shughuli za tume.

Pia shahidi huyo alikiri kupoteza fomu moja ya matokeo ya ubunge katika kata hiyo na nyingine sita za udiwani, lakini akasema baadaye za udiwani zilipatikana.

Awali akiongozwa na wakili wa Serikali (SA) David Kakwaya kutoa ushahidi wake, shahidi huyo alidai kuwa alipokea fomu za matokeo ya vituo vyote 129 katika kata hiyo, lakini baadaye fomu moja ilipotea.

Alisema alikwenda kuangalia fomu ya matokeo aliyokuwa ameibandika ukutani, lakini alibaini kuwa ilikuwa imebanduliwa  na alimuomba  wakala wa Chadema nakala yake ambayo aliitoa kopi.

Shahidi huyo aliwasilisha mahakamani hapo fomu hizo ambazo zilipokewa mahakamani hapo kama kilelezo cha sehemu ya ushahidi wa upande wa utetezi.

Mashahidi wa upande wa madai katika ushahidi wao walidai katika kata hiyo zilipotea fomu tisa za matokeo ya ubunge.

Katika hatua nyingine pia shahidi huyo pia alidai kuwa ziliibuka fujo kubwa katika kituo cha kata baada ya mgombea wa CUF kudai kuwa alikuwa ameshinda kutokana na takwimu zake alizokuwa nazo.

Alidai kuwa mgombea huyo alikataa kabisa kurudia kuhesabu kura pamoja na wafausi wake wakishinikiza atangazwe mshindi jambo lililomlazimu kuita askari polisi ambao walifika na mabomu ya machozi na kumuondoa ofisini hapo chini ya ulinzi mkali.

Mbali na Dk Mahanga wadaiwa wengine katika kesi hiyo ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali(AG) na Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala, ambaye ni Msimamizi wa Uchaguizi wa majimbo ya Ilala.

Mpendazoe anawakilishwa na Wakili Peter Kibatala na  Dk Mahanga anatetewa na Wakili Jerome Msemwa na Wakili Aliko Mwamanenge, huku AG na Mkurugenzi wakitetewa  na Mawakili wa Serikali (SA) David Kakwaya na Seith Mkemwa.

Kesi hiyo itaendelea tena leo mahakamani hapo na  shahidi mwingine wa upande wa madaia ataendelea kutoa ushahidi.

No comments:

Post a Comment