Tuesday, March 27, 2012
Mkurugenzi Tanesco asikitishwa uamuzi wa POAC
MKURUGENZI Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), William Mhando, amesema ingawa suala la kupatiwa umeme lipo kwenye stahili za mkataba wake, hawezi kubishana na uamuzi wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC) wa kuondoa jenereta nyumbani kwake.
Akizungumza kufuatia agizo la POAC kuondoa jenereta hiyo nyumbani kwake jana, ili aonje uchungu wa kukatika kwa umeme, Mhando alisema alishtushwa na hatua hiyo kwa sababu ni suala la mkataba, lakini hawezi kubishana na kamati.
“Mkataba ninao jana (juzi) nilishtuka kuhusu agizo hilo kwa sababu niliajiriwa na bodi na mwenyekiti wangu alikuwapo tutakaa tuangalie, lakini siwezi kupingana na maagizo ya kamati,” alisema Mhando.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa wa Bodi ya Tanesco, Jenerali mstaafu Robert Mboma, alisema watatii agizo la POAC la kuondoa jenereta la dharura lililopo nyumbani kwa mkurugenzi huyo.“Tumeagizwa na kamati tutaangalia jinsi ya kulitekeleza agizo hilo la kuondoa jenereta, tupeni siku tatu au nne hivi mtaona,” alisema Jenerali Mboma.
Alipoulizwa kama kuondoa jenereta hiyo haitakuwa kinyume na mkataba wa ajira unaoonyesha stahili za mkurugenzi huyo, Mboma alisema: “ Unadhani tutafanya nini kama tumeagizwa tuiondoe, hatuna jinsi hata kama kuna mkataba sisi tutatekeleza tuliyoagizwa.”
Mhando alisema suala la kukatika kwa umeme unaondelea hivi sasa, halisababishwi na menejimenti bali inatokana na kutokuwapo kwa uwekezaji muda mrefu kwenye shirika hilo, baada ya kuwekwa chini ya Shirika la Kubinafsisha na Kuuza Mashirika ya Umma (PSRC).
“Tangu mwaka 1999 hadi 2007 hakuna uwekezaji uliofanywa kwa Tanesco baada ya shirika kuwekwa chini ya PSRC, kwa hiyo kukatika kwa umeme kunaokoonekana hivi sasa ni matokeo ya ubinafsishaji uliolengwa,” alisema.
Mkurugenzi huyo alisema kukatika kwa umeme kunatokana na uchakavu wa miundombinu, lakini siyo kuzidiwa na kwenye uzalishaji kwa sababu hivi sasa wanazalisha Megawati 782.51 ilhali mahitaji ni Megawati 772.15.
“Mfano pale City Center (katikati ya jiji), tulikuwa na transfoma mbili zote zimetumika zaidi ya miaka 30, Februari mwaka huu zimeharibika, tumeagiza kutoka Uturuki na sasa zimefika Dubai, tatizo ni miundombinu imechakaa,” alisema.
Kuhusu Aggreko na Symbion Dodoma kuzima mitambo yao, Mhando alikiri kuwa hatua hiyo inatokana na deni ambalo linafikia Sh62 bilioni na kwamba, IPTL imepunguza uzalishaji kutoka Megawati 100 hadi 50. Aggreko inadai Sh58 bilioni na Symbion Dodoma Sh4 bilioni.
“Mgawo kwa maana ya uwezo wa kuzalisha hatuna, ila hii kukatikakatika kwa sababu ya transfoma hiyo ipo. Tupo kwenye hatua mbalimbali za kukarabati miundombinu hiyo na baada ya kipindi tatizo hilo litatoweka,” alisema.
Mhando alisema hivi sasa wamepata dola 85 milioni za Marekani kwa ajili ya Dar es Salaam, Euro 25 milioni kutoka Finland na Benki ya Maendeleo ya Afrika (ADB) imetoa dola 40 milioni za Marekani.
Juzi, Mwenyekiti wa POAC, Zitto Kabwe, alisema lazima jenereta lililoweka nyumbani kwa mkurugenzi huyo liondolewe kwa sababu linatumia mafuta ya Serikali.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment