-Wadai vyama pinzani vimeanza mchezo mchafu
-Mbowe amvaa RC, adai CCM inakaribia kufa
CHAMA Cha
Mapinduzi (CCM), kimeiomba Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), kuwachukulia
hatua za kisheria wanachama na viongozi wa vyama pinzani kwa madai ya
kumdhalilisha mgombea anaewakilisha chama hicho katika uchaguzi mdogo
Jimbo la Arumeru Mashariki, mkoani Arusha, Bw. Sioi Sumari.
Mbunge
wa Simanjiro, mkoani Manyara, Bw.Christopher Ole Sendeka, aliyasema
hayo jana wakati akimnadi Bw. Sumari katika Kata ya Nkoanrua, wilayani
hapa.
Alisema wafuasi wa vyama pinzani jimboni humo wamechana
picha za Bw. Sumari, zingine kupakwa rangi mdomoni 'lipstik', kuzichora
hereni katika masikio na kuzibandika mitaani huku wakijua kufanya hivyo
ni kinyume na taratibu ya uchaguzi.
“Watu wanaofanya hivi
wanaeleweka na wamedhamiria, wanafahamu kuwa kanuni za uchaguzi zinazuia
matendo yasiyofaa kama haya hivyo naiomba NEC ichukue hatua kali.
“Mambo haya yanaweza kusababisha machafuko kwenye kampeni kwani wafuasi wa CCM hawatavumilia matendo haya,” alisema.
Wakati
huo huo, diwani wa Kata ya Ndoombo Nkorisambu, Bw. Wilson Nyiti,
amevitaka vyama vya upinzani kutekeleza kwa vitendo miradi mbalimbali ya
maendeleo.
Alisema viongozi wa vyama hivyo wanawadanganya
wananchi kuwa Serikali ya CCM haijawaletea maendeleo katika kipindi cha
miaka 50 ya uhuru
“Ni vyema wapinzani wakatambua na kuthamini
maendeleo yaliyoletwa na Serikali ya CCM badala ya kupotosha ukweli kwa
mfano, kata hii miaka ya nyuma baarabara zilikuwa hazipitiki lakini
kutokana na juhudi za Serikali, miundombinu imeboreshwa,” alisema Bw.
Nyiti.
Kwa upande wake, Bw. Sumari aliwataka wakazi wa kata hiyo
kuwapuuza wapinzani na kumchagua yeye awe mwakilishi wao bungeni ili
aendeleza mikakati ya maendeleo iliyokuwa ikitekelezwa na marehemu baba
yake, Bw. Jeremiah Sumari.
Katika hatua nyingine, Mwenyekiti wa
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Bw. Freeman Mbowe, amesema
Serikali ya CCM inakaribia kufa kwa sababu ya kutegemea zaidi rushwa na
nguvu ya dola.
Bw. Mbowe aliyasema hayo jana wakati akimnadi
mgombea ubunge wa jimbo hilo kwa tiketi ya chama hicho Bw. Joshua
Nassari, katika mkutano wa kampeni uliofanyika Kijiji cha Maruvango,
kilichopo Kata ya Leguruki.
Alisema CCM imekuwa ikijionesha hadharani jinsi wanavyotumia mabavu hata katika masuala ambayo hayahitaji kutumia nguvu.
“Kuna
kila dalili za chama tawala kufa kutokana na mambo wanayofanya, hii ni
faraja kwetu, sisi tutaendelea kusonga mbele hakuna kurudi nyuma,”
alisema Bw. Mbowe.
Aliongeza kuwa, kitendo cha mfuasi wa CCM
aliyemtaja kwa jina la Bw. Elibariki Kaleria, kumpiga mfuasi wa CHADEMA
Bw. Elia Samweli Nnko (65), kwa sababu ya kuhama chama hicho ni uonevu.
Bw.
Mbowe alimvaa Mkuu wa Mkoa huo Bw. Magesa Mulongo na kudai hajui
majukumu yake kwa sababu ya kuacha ofisi badala yake amekimbilia Kata ya
Kingori kumnadi mgombea ubunge wa CCM.
“Namsihi Bw. Mulongo
aache kutumia kofia aliyonayo vibaya, achague moja kama ni siasa au Ukuu
wa Mkoa ili atumikie wannchi akiwa ofisini kwake,” alisema Bw. Mbowe.
No comments:
Post a Comment