SIKU chache baada ya Rais Jakaya Kikwete kuagiza maaskari wanaokiuka
maadili ya Jeshi la Polisi na kulipaka matope kuchukuliwa hatua ikiwamo
kufukuzwa kazi, polisi mkoani Kilimanjaro amekamatwa akidaiwa kufanya
vurugu disko huku akiwa na misokoto minne ya bangi.
Katika tukio hilo, polisi huyo wa kituo cha Majengo mjini hapa, G842
Konstebo Deogratius, anashikiliwa na Polisi baada ya kufanya fujo
katika ukumbi wa disko wa Pub Alberto.
Akithibitisha jana kukamatwa kwa askari huyo, Kamanda wa Polisi wa
Mkoa, Absalom Mwakyoma, alisema askari huyo alikutwa akifanya vurugu
Jumamosi saa mbili usiku ukumbini humo. Mwakyoma alidai askari huyo
alikwenda hapo kunywa pombe na kucheza muziki na wakati muziki
unaendelea, mlinzi wa eneo hilo alipewa taarifa na wateja kuwa kuna
mmoja wa wachezaji anawafanyia fujo.
Alidai kuwa mlinzi huyo aliyejulikana kwa jina la Rajab Hamad
alipokwenda na kumtuliza askari huyo, aling’atwa mkononi, ndipo mmiliki
wa ukumbi huo, Christopher Shayo ‘Chris Burger’ alipotaka kujua
kulikoni na kuambulia ngumi ya usoni kutoka kwa askari huyo.
Kamanda aliongeza kuwa baada ya vurugu hizo, askari walifika eneo la
tukio na kumkamata askari huyo ambaye alipekuliwa, na kukutwa na
misokoto hiyo ya bangi mfukoni. Alisema mtuhumiwa aliwekwa mahabusu
wakati upelelezi ukiendelea na hatua nyingine za kinidhamu dhidi yake
zitafuata.
Aliongeza kuwa watu wote walioshambuliwa ikiwa ni pamoja na mmiliki
wa ukumbi huo na walinzi wake wawili walipewa fomu ya matibabu ya PF3
na kwenda kutibiwa hospitalini na hali zao zinaendelea vizuri.
Matukio ya askari kufanya vitendo vinavyokwenda kinyume na maadili
ya Jeshi hilo, vimeonekana kushika kasi mkoani humo. Hili ni tukio la
pili katika miezi michache ya mwaka huu baada ya lile la askari mwingine
kuingia ukumbi huo akiwa na bunduki aina ya SMG na kuwafanyia watu
fujo.
No comments:
Post a Comment