SIKU chache kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mdogo wa ubunge Arumeru
Mashariki, vyama vyenye ushindani mkali katika uchaguzi huo, CCM na
Chadema, vimeanza kutupiana maneno.
CCM jana ilitoa shutuma mpya kuwa Chadema inasambaza taarifa kwa
wananchi kwamba mgombea wake, Sioi Sumari, amejitoa kwenye
kinyang’anyiro hicho, huku wafuasi wanaodaiwa kuwa wa Chadema wakichora
picha mbaya za mgombea huyo wa CCM. Chadema nao pamoja na kukana
taarifa hiyo, wamedai kuwa CCM mikutano yao imejaa matusi.
Siasa chafu Chadema Akihutubia wakazi wa kijiji cha Usa River
katika mkutano wa hadhara kwenye uwanja wa michezo wa Ngaresero juzi
jioni, Meneja wa Kampeni za CCM, Mwigulu Nchemba alidai Chadema wameanza
kufanya siasa chafu katika mikutano ya kampeni iliyofanyika juzi.
Nchemba alidai kwamba viongozi wa Chadema wakifanya kampeni katika
kijiji cha Leguruki waliwatangazia wananchi, kwamba watakuwa na kazi
rahisi ya kuchagua mbunge kwa kuwa mgombea wa CCM ameshajitoa.
“Ndugu wananchi jambo hili linadhihirisha kauli yangu, kwamba
viongozi wa Chadema na hasa Dk. Slaa (Willibrod – Katibu Mkuu) wameanza
kuchanganyikiwa, na muda si mrefu wataanza kuokota makopo,” alidai
Nchemba. Alidai CCM ilitambua, kwamba Chadema wangeweza kufanya hivyo
Jumapili kutokana na Aprili mosi kuwa Siku ya Wajinga, lakini wameamua
kufanya hivyo mapema jambo ambalo alisema halikubaliki.
“Haya ni mambo ya ajabu sana. Wanazunguka vijiji vyote na helikopta
kutangaza kuwa mgombea wetu kajitoa, wanasema kajitoa lakini Sioi si
huyu hapa mnamwona?” Alihoji Nchemba.
Aliwataka wananchi kuwa macho na propaganda hizo alizosema
zinatokana na Chadema kubaini kuwa watashindwa katika uchaguzi huo na
hivyo kutafuta mbinu zitakazofanya wananchi kuhadaika na kumpigia kura
mgombea wa Chadema, Joshua Nassari.
Akizungumza katika mkutano huo, Sioi alisema anajivunia kugombea
ubunge kutoka katika chama kinachounda Serikali kwa kuwa na utajiri wa
watendaji, kuanzia Rais, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu, mawaziri, naibu
mawaziri, wakuu wa mikoa na wilaya ambao alisema watakuwa msaada mkubwa
katika utendaji wake wa kazi.
“Ndugu wananchi juzi alikuwepo hapa Mzee Stephen Wassira, ambaye ni
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais anayeshughulikia Sera, Uratibu na
Uhusiano… siku mkinichagua nitamfuata nyumbani na kukataa kutoka
sebuleni hadi asikilize kilio chenu,” alisema Sioi.
Alisema pamoja na kubuni vyanzo vya ajira kwa vijana, pia
atahakikisha madereva wa bodaboda wanawezeshwa kwa kupewa vitendea kazi
na mitaji itakayowawezesha kukuza biashara na kuinua biashara zao.
No comments:
Post a Comment