WIZARA ya Kilimo na Maliasili imezindua kanuni ambazo zitadhibiti
matumizi ya misumeno ya moto kwa ajili ya kukabiliana na kasi ya
uharibifu wa mazingira inayotokana na ukataji wa miti uliokithiri.
Hatua hiyo imekuja baada ya kuwepo kwa wimbi la ukataji wa miti
mbalimbali ikiwemo ya matunda kwa matumizi ya mbao na ujenzi kwa kutumia
misumeno ya moto, zaidi vijijini Unguja na Pemba.
Akizindua kanuni hizo, Kaimu Waziri wa Kilimo na Maliasili Ramadhan
Abdalla Shaaban alisema hivi sasa kuna kasi kubwa ya ukataji wa
rasilimali za misitu kwa kiwango kinachotishia mazingira ya uhai wa
miti.
Shaaban alisema kwa mwaka, hekta za misitu 950 zinakatwa bila ya
kuzingatia suala zima la upandaji wa miti mipya kwa ajili ya matumizi
mbalimbali.
Alisema Wizara imeamua kutunga kanuni mpya zitakazodhibiti matumizi
mabaya ya ukataji wa misitu kutokana na kuwepo kwa misumeno ya moto.
“Zanzibar inakabiliwa na kiwango cha kutisha cha ukataji wa misitu
usiozingatia uhifadhi wa mazingira, ndiyo maana tumetunga kanuni mpya za
kudhibiti ukataji wa miti kutokana na kuwepo kwa matumizi ya misumeno
ya moto,” alisema Shaaban.
Alisema kuanzia sasa mtu yeyote atakayemiliki msumeno wa moto,
atalazimika kuomba maombi rasmi yatakayomhalalishia kumiliki msumeno huo
baada ya kukubaliwa na idara husika ya ardhi.
Shaaban alisema adhabu kali itamkabili mtu atakayemiliki msumeno wa
moto bila ya kibali husika ikiwemo kwenda chuo cha mafunzo jela miezi
sita au kulipa faini Sh 300,000.
Viongozi waandamizi wa wizara hiyo wakifuatana na watendaji wa Idara
ya Misitu walishiriki katika uchomaji moto misumeno iliyokamatwa na
maofisa wa idara hiyo ambayo ilikuwa ikifanya kazi kinyume cha sheria
kukata miti katika maeneo mbalimbali ikiwemo misitu ya Hifadhi ya
Serikali.
Mapema Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini Unguja, Riziki Simai alikiri
kuwepo kwa kasi ya ukataji wa miti ikiwemo minazi pamoja na miembe kwa
matumizi ya mbao na ujenzi.
No comments:
Post a Comment