ALIYEKUWA Mkuu wa Kituo cha Polisi cha Buguruni, Mark Njela (37)
ameieleza Mahakama kuwa hakupokea taarifa za aliyekuwa Mgombea wa Ubunge
katika Jimbo la Segerea kupitia CCM, Dk Milton Mahanga kukamatwa na
masanduku ya kura.
Aidha alidai kuwa hakuna matukio ya jinai yaliyotokea katika
Uchaguzi Mkuu wa mwaka juzi, likiwemo tukio la kuchomwa kwa Ofisi ya
Mtendaji wa Kata ya Kiwalani iliyokuwa ikitumika kufanya majumuisho ya
kura katika kata hiyo.
Njela, ambaye ni Mkuu wa Upelelezi wa Wilaya ya Kati ya kipolisi,
alidai hayo jana katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam wakati
akitoa ushahidi katika kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa jimbo hilo
yaliyomtangaza Dk Mahanga kuwa mshindi.
Mwaka juzi mgombea ubunge wa jimbo hilo kupitia Chadema, Fred
Mpendazoe alifungua kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa jimbo hilo
dhidi ya Dk. Mahanga, Mwanasheria Mkuu wa Serikali na aliyekuwa
msimamizi wa uchaguzi wa jimbo hilo kwa madai kuwa uchaguzi huo ulikiuka
matakwa ya sheria ya uchaguzi ya mwaka 2010.
Akitoa ushahidi baada ya Wakili Seth Mkemwa kumuonesha gazeti la
Mwananchi lililoripoti Dk Mahanga amekamatwa na masanduku ya kura katika
eneo la Buguruni, Njela alidai alisikia taarifa hiyo na kuna mwandishi
wa habari alimpigia simu lakini hakuna jalada lililofunguliwa.
“Hizi ni taarifa tu na ndio maana hata Kamanda wa Polisi Kanda ya
Dar es Salaam, Suleiman Kova alijibu ofisi yake haina taarifa kwa
sababu hakukuwa na tukio hilo na sisi ndio huwa tunampelekea taarifa
hivyo na mimi najibu sina taarifa hizo,” alidai.
Wakili wa mdai, Peter Kibatala alimuuliza Njela kama amewahi kupokea
taarifa zozote za matukio ya jinai zilizotokea katika kipindi cha
uchaguzi, Njela alijibu hakupokea taarifa yeyote.
Alipoulizwa kuhusu tukio la kuchomwa kwa Ofisi ya Mtendaji wa Kata
ya Kiwalani ambayo ilikuwa ikitumika kufanya majumuisho ya kura, Njela
alidai alisikia lakini hakuthibitisha na tukio hilo halikuripotiwa
katika kituo chake.
Kibatala alimuuliza Njela kama ni kweli Jeshi la polisi limekuwa
likilalamikiwa sana na nchini kwa kutotenda haki na kuna ripoti nyingi
zinaeleza jinsi polisi wanavyopendelea upande mmoja, Njela alijibu si
kweli.
Alipoulizwa kama alipandishwa madaraka miezi saba baada ya uchaguzi,
Njela alikiri kupandishwa madaraka kutoka Mkuu wa Kituo hadi kuwa Mkuu
wa Upelelezi wa Wilaya ya Kati, huku akidai kupandishwa madaraka
kulitokana na ufanisi wake wa kazi.
No comments:
Post a Comment