MUASISI wa Chadema, Edwin Mtei ameamua kuvunja ukimya na kuzungumzia
kauli ya mbunge Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe ya kutangaza nia ya
kugombea urais mwaka 2015.
Amekosoa uamuzi wa mbunge huyo kwa madai kwamba amefanya mapema mno kutangaza nia yake.
Amesisitiza
kwamba Chadema hawawezi kumchagua mtu aliyejitangaza mapema kuwania
urais bali watatumia vigezo vya uadilifu na uwajibikaji kupitia vikao
halali vya chama.
“Bado miaka mitatu,ni mapema sana, hatuwezi
kumchagua mtu aliyejitangaza mapema. Tutamchagua mtu kwa vigezo. Ni
vizuri angesubiri vikao vya chama ndipo azungumze” alisema Mtei.
Mtei
ambaye aliwahi kuwa Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) alivunja
ukimya huo jana wakati akihojiwa na gazeti hili kuhusu kauli ya Zitto
inayoonekana kuwachanganya watendaji wakuu wa chama hicho.
Juzi,
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe pamoja na Katibu Mkuu wake, Dk
Willibrod Slaa walitoa maoni yao tofauti juu ya kauli hiyo ya Zitto.
Dk
Slaa alikosoa hatua hiyo na kusema siyo wakati mwafaka sasa kuzungumzia
urais, lakini Mbowe alisema hana tatizo na Zitto kutangaza nia hiyo kwa
kuwa ni haki yake, lakini akahoji haraka ya kutangaza dhamira hiyo.
Hatahivyo,kwa
nyakati tofauti viongozi hao walimshauri Zitto kufuata taratibu za
chama kama anataka kufikia malengo yake hayo ya kutaka kuwania nafasi
hiyo ya juu kabisa ya uongozi wa taifa.
Akihojiwa ,
Mtei alisema kwamba ni mapema sana kwa mwanachama wa Chadema kuelekeza
akili yake ya kuwania urais kupitia chama hicho wakati muda bado
haujafika.
Alisisitiza kwamba ni mapema sana kwa kuwa kuna watu
ambao bado hata hawajaingia ndani ya Chadema na kujulikana kwa sasa
hivyo alishauri wenye mawazo hayo kusubiri hadi muda uwadie.
Akizungumza
kwa hisia muasisi huyo alibainisha ya kwamba kila mtu ndani ya Chadema
ana msimamo wake lakini ni mapema sana mtu au kiongozi ndani ya chama
hicho kuelekeza akili yake kuwania nafasi ya urais.
“Kila mtu ana
msimamo wake ila tunasema ni mapema kusema mtu kuzungumzia nani
atateuliwa na chama sasa ni mapema mno,”alisisitiza Mtei
No comments:
Post a Comment