KAMATI ya Hesabu za Mashirika ya Umma(POAC), imeagiza Bodi ya Shirika la
Umeme Tanzania (Tanesco) kuondoa jenereta la dharura lililopo nyumbani
kwa Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo, William Mhando kuanzia leo ili naye
ajue machungu ya kukatika umeme mara kwa mara.
Wakati POAC
ikiagiza kuondolewa kwa jenereta hilo, taarifa zinaeleza kuwa Mwenyekiti
wa Bodi ya Tanesco, Jenerali Mstaafu, Robert Mboma amemwandikia Waziri
wa Nishati na Madini, William Ngeleja akihoji sababu za kutokutekelezwa
kwa agizo la Rais Jakaya Kikwete la kulipatia shirika hilo kiasi cha
Sh408 bilioni kwa ajili ya kujiendesha.
Barua ya Mboma ya Machi 20,
mwaka huu kwenda kwa Ngeleja, ambayo gazeti hili imefanikiwa kuiona,
ilisema mnamo Machi, 8 mwaka huu, Rais Kikwete aliagiza Tanesco ipewe
haraka mkopo huo wa Sh408 bilioni lakini akasema hadi sasa amri hiyo ya
Amiri Jeshi Mkuu haijatimizwa.
“Mheshimiwa Rais tarehe 8 Machi
aliagiza kuwa mkopo huo wa Sh408 bilioni upatikane haraka. Lakini, sisi
tunazunguka na hivyo kushindwa kutii amri ya Amiri Jeshi Mkuu wa
Tanzania. Katika hali ya kawaida, tunatakiwa tufanyekazi usiku na mchana
kwa nia ya kukamilisha maagizo halali ya Rais wa Jamhuri ya Muungano,"
inasema sehemu ya barua hiyo ya Mboma.
Katika sehemu nyingine ya
barua hiyo, Mboma alisisitiza: "Hali ya mabwawa yanayotegemewa ya Mtera
na Nyumba ya Mungu ni mbaya sana. Ukosefu wa mafuta utatulazimu tutumie
maji hayo... hii maana yake ni kuwa mwakani tutalazimika kukodi mitambo
mingine ya dharura kwa sababu mitambo ya sasa, muda wake utakuwa
umekwisha. Watanzania hawatatuelewa na Tanesco italaumiwa bure kwa
sababu tuko ambao hatutii amri za ngazi za juu."
Mboma katika
kuhakikisha agizo hilo la Rais linatekelezwa, aliomba kikao kati yake na
Waziri Ngeleja, Katibu Mkuu wa Nishati na Madini, wajumbe wawili wa
bodi, menejimenti ya shirika hilo na wajumbe wengine ambao waziri huyo
angeona wanafaa.
“Lengo liwe ni kutafuta njia za kufanya ili
turekebishe kasoro. Wakati huohuo; napendekeza Katibu Mkuu wetu
azungumze na mwenzake wa Hazina. Hii iwe baada ya menejimenti ya Tanesco
kumjulisha juu ya mazungumzo yao,” ilisisitiza barua hiyo na kuongeza:
“Itapendeza
kama Katibu Mkuu (WNM) atakuwa amezungumza na mwenzake wa Hazina kabla
ya kikao chetu. Baada ya hapo, naona tuone jinsi ya kuzungumza na
mheshimiwa Rais. Suala hili ni zito."
Nakala ya barua hiyo
ilipelekwa pia kwa Katibu Mkuu Kiongozi, Ofisi ya Rais, Katibu Mkuu
Wizara ya Fedha, Katibu Mkuu Nishati na Madini, Msajili Hazina na
Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco.
Msimamo wa POAC
Mwenyekiti
wa POAC, Zitto Kabwe akizungumzia suala la jenereta alisema ni lazima
liondolewe kwa kuwa linatumia mafuta ya Serikali na ndiyo maana
mkurugenzi huyo hawezi kujua adha iliyopo kwa wananchi pindi umeme
unapokatika.
“Tumemtaka Jenerali Mboma afanye hivyo kwa kuwa
haiwezekani mkurugenzi wa huyo awekewe jenereta kwani kwa kufanya hivyo
inadhihirisha kwamba hawana umeme wa uhakika,” alisema.
Zitto
alisema wameagiza hilo lifanyike haraka na kama mkurugenzi huyo anataka
kuwa na jenereta anunue la kwake binafsi na si kutumia la umma na mafuta
ya Serikali.
Alisema Tanesco imeendelea kuelemewa na mzigo wa
kununua umeme kutoka makampuni binafsi na imepata hasara ya Sh47 bilioni
kutoka Sh43 bilioni mwaka 2009.
Zitto alisemza mwaka 2010,
Tanesco ilitumia kiasi cha Sh211 bilioni kununua umeme wa dharura kutoka
kampuni binafsi na asilimia 90 ya fedha hizo zimetumika kwa Songas na
IPTL… “Songas wametumia kiasi cha Sh127 bilioni na Sh64 bilioni
zimetumika kwa IPTL.”
Alisema kutokana na hali hiyo wameitaka Tanesco
kuanzia Mei mwaka huu, waache kutumia mitambo ya IPTL baada ya mtambo
wao mpya wa Jacobsen unaojengwa Ubungo, Dar es Salaam kuanza kufanya
kazi na kuzalisha megawati 100.
Zitto alisema hivi sasa Tanesco
wamepunguza gharama za uendeshaji lakini wanatumia Sh499 bilioni
kuzalisha na umeme ambao wakiuza wanapata Sh466 bilioni na ukiongeza
gharama nyingine za mishahara unakuta wanapata hasara ya Sh47 bilioni
kila mwaka.
Kuhusu kuwepo kwa mgawo wa umeme Zitto alisema
Tanesco imekubali kuwa kuna mgawo usio rasmi na hiyo inatokana na kukosa
dhamana kutoka serikalini ya kupata mkopo wa Sh408 bilioni ili iweze
kununua umeme wa dharura na kuondokana na tatizo la umeme.
Zitto
ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), alisema hali ndani
ya shirika hilo ni mbaya kwa sababu haina fedha za kuliendesha na kwamba
hawawezi kununua vipuri.
Alisema kutokana na hali hiyo umeme
unaokatikakatika ni mgawo lakini shirika hilo limekuwa likikanusha kwa
sababu uwezo limekuwa likipokea malalamiko mengi yanayohusu ukatikaji
huo hasa Dar es Salaam.
“Hali ya mabwawa kwa mujibu wa taarifa ya
Mwenyekiti wa Bodi ya Tanesco, Jenerali Mboma inaeleza kuwa ni mbaya
kwani Mtera lina mita 1.24 tu juu ya kiwango cha chini kinachoruhusiwa
na sasa bado mita 5.26 kufikia kima chake cha juu,” alisema Zitto na
kuongeza:
“Nyumba ya Mungu ina mita 3.22 juu ya kina cha chini
kinachoruhusiwa na ni mita 9.76 kufikia kina cha juu cha bwawa hilo
hivyo maji kwenye mabwawa hayo ni kidogo hasa kama mvua haitanyesha
maeneo ya Mbeya Dodoma, Arusha Kilimanjaro, Singida na Tanga.”
Alisema
ukosefu wa fedha za kununulia mafuta utalazimu watumie maji hayo kidogo
ili wasifanye mgawo wa umeme na hiyo maana yake ni kuwa mwakani
watalazimika kukodi mitambo mingine ya dharura kwa sababu ya sasa muda
wake utakuwa umekwisha.
Zitto alisema kutokana na hali hiyo,
wamemwagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini kushughulikia
suala hilo ili fedha hizo zipatikane.
“Mtambo wa Aggeko umezimwa na IPTL pia ambayo yote kwa ujumla huzalisha megawati 150,” alisema.
Awali,
kabla ya kuhojiwa na POAC Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco, Mhandisi William
Mhando alisema tatizo la umeme katika Mkoa wa Dar es Salaam litakwisha
baada ya wiki nne kwa kuwa wahandisi wa shirika hilo wanafanyia kazi
matatizo yaliyopo.Alisema kukatika umeme mara kwa mara hasa maeneo ya
Mbagala, Temeke na Kigamboni kunatokana na mfumo wa umeme uliopo
kuchakaa na ili kutatua tatizo hilo wameagiza transfoma nne za dharura.
“Hali
ya umeme si mbaya tunamudu mahitaji kwa kutumia maji japokuwa si mengi
na pia tunatumia gesi. Mifumo yetu ya umeme si mizuri kwa kuwa
imechakaa,” alisema Mhando.
No comments:
Post a Comment