KAMATI ya Hesabu za Serikali Kuu (PAC), haikuridhishwa na hesabu za
Wizara ya Mambo ya Ndani baada ya kubaini kuwapo upungufu uliosababisha
kupata hati yenye mashaka kipindi cha miaka mitatu mfululizo.
Akizungumza
kwenye kikao cha kamati hiyo Dar es Salaam jana, Kaimu Mwenyekiti wa
kamati hiyo, Ezekiah Chibulunje, alisema baada ya kamati kupitia vitabu
vya wizara wamebaini kuwapo kwa matatizo kwenye hesabu na kusababisha
baadhi ya fedha kutoonekana matumizi yake.
“Kamati haikuridhishwa
na hesabu za wizara, hii ni mara ya kwanza kuona hesabu hazieleweki na
wala hakuna kumbukumbu za kutosha tangu tulipoanza kupitia hesabu za
wizara mbalimbali nchini,” alisema Chibulunje.
Alisema tatizo
hilo linatokana na kuwapo kwa Mhasibu Mkuu mwenye elimu ya Diploma,
ambayo imesababisha kushindwa kuweka kumbukumbu za matumizi ya fedha
vizuri wakati Serikali inawataka wahasibu wakuu kuwa na elimu ya kiwango
cha CPA.
Chibulunje alisema mhasibu huyo ameshindwa kutoa
maelezo ya kueleweka kwenye kamati kuhusu matumizi ya fedha za Serikali
na miradi ya wizara, jambo ambalo limesababisha kupata hati yenye
mashaka kipindi chote.
Alisema kutokana na hali hiyo, kamati
imeitaka wizara kukaa na wakaguzi kutoka Wizara ya Fedha na Uchumi
kitengo cha hazina, ili kukagua hesabu zao na kutoa maelekezo ya
upungufu uliojitokeza uweze kufanyiwa marekebisho.
Hata hivyo, Katibu
mkuu wa wizara hiyo, Mbaraka Abdulwakil, alikiri kuwapo kwa upungufu
huo na kudai kuwa, umetokana na mfumo wa mtandao uliosababisha baadhi ya
hesabu kutoonekana.
Abdulwakil alisema wakati hazina imeanzisha
mfumo mpya, walipata tatizo la kuziingiza fedha hizo jambo ambalo
limesababisha baadhi ya fedha kutoonekana kwenye vitabu hivyo.
No comments:
Post a Comment