-Wasema hawana hofu ya Mungu, wakerwa na malumbano
VIONGOZI serikalini wameshauriwa kuacha kupoteza muda mwingi katika
malumbano wakati Watanzania wakizidi kukabiliwa na hali ngumu ya maisha
licha ya Taifa kuwa na rasilimali nyingi.
Mchungaji wa Huduma ya
Hossana Alive Vision, Ephraim Mwansasu, aliyasema hayo Dar es Salaam
jana wakati akizungumza kwa niaba ya wachungaji wenzake kwenye mkutano
wa injili uliofanyika Mtoni Kijichi.
Alisema viongozi wengi serikalini, wanatumia muda mwingi kulumbana na wanasiasa waakati nchi inakabiliwa na changamoto nyingi.
“Umefika
wakati wa wachungaji wote nchini kuungana ili kuliombea Taifa hili
ambalo hivi sasa limepoteza mwelekeo kwa sababu ya uovu uliokithiri.
“Serikali
iliyopo madarakani iangalie upya mwelekeo wa nchi yetu, kuacha
malumbano na vyama vya siasa,” alisema Mchungaji Mwansasu na kuongeza
kuwa, ipo haja ya Serikali kujipanga ili kuhakikisha inatatua matatizo
yanayowakabili Watanzania.
Alisisitiza kuwa, Serikali ya Aawamu
ya Nne ina viongozi wengi ambao hawana hofu ya Mungu moyoni mwao ndiyo
maana kuna ufisadi mwingi.
Katika hatua nyingine Mchungaji
Mwansasu aliwataka Wakristo kote nchini kumgeukia Mungu ili waweze
kufanya mambo ya kumpendeza yeye na kufuata maagizo yake.
Alisema nyakati za sasa ni za mwisho ndiyo maana maasi yamekuwa mengi hivyo ni vyema Wakristo wakawa karibu na Mungu.
No comments:
Post a Comment