PAMOJA na Shirika la Umeme (Tanesco) kudai kuwa kukatikakatika kwa umeme
kunakoendelea, kunatokana na shirika hilo kuzima mitambo ya Aggreko,
taarifa ya uzalishaji wa umeme kwenye Gridi ya Taifa, imeonesha kuwa
umeme unaozalishwa unatosha na kuzidi mahitaji.
Taarifa ya uzalishaji umeme kwa jana ambayo gazeti hili linayo,
ilionesha kuwa umeme uliokuwa ukizalishwa katika Gridi ya Taifa bila
kuwashwa kwa mitambo hiyo, ni megawati 742.60 wakati mahitaji halisi ya
umeme ni Megawati 683.
Akifafanua hali hiyo ofisini kwake jana, Kamishna wa Nishati katika
Wizara ya Nishati na Madini, Prosper Victus, alisema katizo la umeme la
mara kwa mara linatokana na kuzeeka kwa mitambo ya kusambaza umeme ya
Jiji la Dar es Salaam.
Wakati Victus akitoa taarifa hiyo, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya
Hesabu za Masharika ya Umma (POAC), Kabwe Zitto (Chadema), alidai kuwa
Tanesco wamedai kuwa umeme unakatika kutokana na kuzimwa kwa mitambo ya
Aggreko kulikosababishwa na kukosa fedha za kuendesha mitambo hiyo.
Zitto aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa shirika hilo
limeshindwa kupata fedha za kuendesha mitambo ya Aggreko kutokana na
Serikali kushindwa kutoa Sh bilioni 408 kwa Tanesco.
Fedha hizo ziliahidiwa kutolewa na Serikali ili kuisaidia
kukabiliana na mpango wa dharura wa kuzalisha megawati 200 ambazo
zinazalishwa kwa pamoja kati ya Aggreko na kampuni ya kufua umeme wa
gesi ya Symbion. Kila kampuni inazalisha megawati 100.
“Tumeiagiza Serikali itoe fedha hizo ili kuepusha nchi kuingia
kwenye mgawo mkubwa,” alisema Zitto ambaye katika kikao cha jana
aliwazuia waandishi wa habari kushiriki kwenye majadiliano kati ya
kamati na viongozi wa Tanesco.
Hata hivyo, Victus alifafanua kuwa mitambo hiyo imezimwa kwa kuwa
hali ya uzalishaji wa umeme inaridhisha na umeme uliopo unapita mahitaji
na mitambo iliyozimwa, ni kwa sababu ya akiba na itawashwa pale
panapotokea ulazima wa kuiwasha.
Zitto alisema Kamati yake iliwahoji kwa kina maofisa wa Serikali
wakiongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi
kutaka kujua sababu ya kukatika mara kwa mara kwa umeme ambao
walijitetea kuwa ni matatizo ya kiufundi.
“Lakini Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco (William Mhando) alipobanwa
alisema tatizo hilo linatokana na kuzimwa kwa mashine za Aggreko,”
alisema Zitto na kuongeza kuwa hadi jana Tanesco wanadaiwa zaidi ya Sh
bilioni 230 na Aggreko.
Licha ya kuanza utekelezwaji wa mpango wa dharura, matatizo ya umeme
bado yameendelea kuikumba nchi kutokana na kukatika mara kwa mara kwa
nishati hiyo.
Jijini Dar es Salaam hasa maeneo ya katikati ya mji hali ni mbaya
nyakati za mchana kutokana na maeneo hayo kukosa umeme kila siku mchana.
Mwenyekiti huyo wa POAC alisema katika kupitia hesabu za Tanesco
wamebaini kuwa shirika hilo liko taabani kifedha baada ya kupata hasara
ya Sh bilioni 47 katika hesabu za mwaka 2010.
Akichambua hesabu hizo, Zitto alisema hasara hiyo inatokana na
shirika hilo kutumia fedha nyingi kuyalipa makampuni ya Songas na IPTL
ambayo yanaliuzia shirika hilo umeme.
Alitoa mfano kuwa mwaka 2010 Tanesco ilitumia Sh bilioni 211 kuilipa
IPTL na Sh bilioni 126.9 kuilipa Songas kama malipo ya kununua umeme
kutoka kwa kampuni hizo. “Suluhisho hapa ni kupunguza kununua umeme kwa
IPTL ili shirika lipate faida…wakiachana na IPTL watapata faida,”
alisema Zitto.
Alifafanua kuwa jumla Tanesco inatumai Sh bilioni 492.25 kama
gharama za kununulia umeme wakati mapato yake ni Sh bilioni 466.77 kwa
mwaka. Mbunge huyo alisema wameiagiza Tanesco kuhakikisha ifikapo Mei
isitishe kununua umeme kutoka IPTL badala yake waharakishe kukamilisha
mtambo wao wa kuzalisha megawati 100 unaosimikwa Ubungo.
Alisema Tanesco ikiachana na IPTL, itapata faida kwani IPTL
inalinyonya shirika hilo fedha nyingi kuliko gharama za umeme
wanaozalisha. Alisema licha ya mapato hayo, Tanesco inapokea Sh bilioni
106 kama ruzuku kutoka serikalini lakini shirika hilo linatumia fedha
hizo kununua umeme pamoja na kulipa madeni hali inayolifanya lijikute
limepata hasara hiyo ya Sh bilioni 47.
Wakati huo huo, kamati hiyo imemwamuru Mhando kung’oa jenereta
analotumia na kulipiwa gharama na Tanesco. Uamuzi huo unatokana na madai
kuwa Mkurugenzi huyo hapatwi na machungu ya mgawo wa umeme kwani
jenereta hilo linatoa umeme muda wote mara tu ukikatika.
“Nimemwagiza Jenerali Mboma (Robert) ambaye ni Mwenyekiti wa Bodi
ahakikishe jenereta hilo linang’olewa, la sivyo Mkurugenzi huyo
ajigharimie mwenyewe mafuta na si kulipiwa na Tanesco,” alisema Zitto.
No comments:
Post a Comment