Mwenyekiti wa LAAC, Augustine Mrema
KAMATI
ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), imeibua tuhuma za
ufisadi wa Sh2.7 bilioni katika mradi wa ujenzi wa machinjio ya kisasa
Gongo la Mboto, Dares Salaam uliopaswa kufanywa na Kampuni ya East
Africa Meat (EAMC).Mradi huo ulipaswa kutekelezwa kati ya mwaka 2005/06 kwa ushirikiano wa jiji na Manispaa tatu za Dar es Salaam.
Akizungumza
Dar es Salaam jana kwenye kikao kati ya kamati yake na watendaji wa
Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, Mwenyekiti wa LAAC,
Augustine
Mrema alisema kampuni hiyo ya Malaysia ndiyo iliyoshinda zabuni ya
ujenzi wa machinjio hayo.
Mrema alisema katika mradi huo,
Halmashauri ya Jiji iliingia mkataba wa kughushi na EAMC, huku
wakiwashawishi watendaji kushiriki kwenye ujenzi wa machinjio hayo
yanayodaiwa kuwa ya kisasa.
Alisema kutokana na hali hiyo Halmashauri
ya Kinondoni ilitoa Sh229milioni wakati ya Ilala ilitoa Sh364miloni,
Temeke ilitoa Sh224milioni huku jiji likitoa Sh1.2bilioni.
Alisema
kutokana na hali hiyo, fedha hizo zimepelekwa kwenye miradi huo ambao
mpaka sasa haujatekelezeka jambo ambalo linaonyesha kuwa kuna baadhi ya
wajanja ambao wamechukua fedha hizo.
“Tunajua kabisa kuwa kuna
baadhi ya vigogo wameshiriki kuwarubuni watendaji wa halmashauri kwa
ajili ya kutekeleza miradi hewa, hatutakubali na kila aliyeshiriki
atachukuliwa hatua za kisheria,” alisema Mrema.
Alisema mbali na
hilo, baadhi ya vigogo hao ndiyo walioshiriki kwenye kashfa ya Shirika
la Usafiri Dar es Salaam (UDA), ambalo ripoti yake bado inasubiriwa
ikabidhiwe serikalini kutoka kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za
Serikali (CAG).
Mrema alisema kutokana na hali hiyo, LAAC
itawasilisha taarifa hizo kwa watendaji wakuu ili waweze kuangalia hatua
stahiki za kurudishwa kwa fedha hizo katika halmashauri ikiwa ni pamoja
na kuwafikisha mahakamani wahusika walioshiriki kwenye utapeli huo.
“Haiwezekani
hata kidogo watu wachache wanufaike na rasilimali za taifa kwa manufaa
yao, jambo ambalo limesababisha kuingia mikataba feki ambayo wanajua
kabisa kuwa haiwanufaishi wananchi. Lazima fedha hizi zirudi,” alisema.
Meya: Kampuni imefilisika
Hata
hivyo, Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Dk Didas Masaburi alisema kampuni
hiyo imefilisika na kwamba hakuna mtu atakayeweza kulipa deni hilo.
Kutokana na hali hiyo, alisema watakaa na halmashauri za manispaa ili
kuangalia jinsi ya kutatua matatizo hayo.
“Kampuni yenyewe
imefilisika, nani atalipa deni hilo? Hakuna kwa sababu hata jiji ni
miongoni mwa watu waliotapeliwa japo tulikuwa tumeingia ubia lakini
kilichofanyika ni kwamba mradi huo haujatekelezeka,” alisema Dk
Masaburi.
Alisema machinjio hayo yalitakiwa kujengwa mwaka 2006, lakini mpaka sasa hayajengwa na wala hakuna eneo la ujenzi.
Meya
Masaburi alisema halmashauri hizo zilitoa fedha hizo na kudaiwa kuwa
zimetumika kwenye upembuzi yakinifu na kuongeza kwamba, ilipofika mwaka
2009, madiwani wa jiji na manispaa walitaka ufafanuzi kuhusu suala hilo
na kuitaka jiji kujiondoa kwenye mkataba huo jambo ambalo lilisababisha
halmashauri hizo kudai fedha zao ambazo mpaka sasa hazijalipwa.
Alisema
wakati hayo yakiendelea, tayari kampuni hiyo ilikuwa imefilisika na
hakuna mtu mwenye uwezo wa kuendelea na mkataba au kurudisha fedha.
“Meneja
wa kampuni hiyo ambaye ni raia wa Zimbabwe aliyejulikana kwa jina la
Benjamin Chipazi ni miongoni mwa watu waliotapeliwa, anadai mafao yake
ya zaidi ya Dola za Marekani 150,000, lakini ameshindwa kulipwa kwa
sababu hakuna mtu aliyerithi madeni hayo,” alisema.
Alisema
kutokana na hali hiyo, jiji haliwezi kurithi madeni ya kampuni hiyo na
kwamba kila mmoja anapaswa kutambua kuwa katika mkataba huo
wametapeliwa.
Iddi Simba Mwenyekiti
Alipoulizwa jana, Mwenyekiti wa EACM, Iddi Simba alikiri kuwa kampuni hiyo na ilikuwa ijenge mradi huo.
Alisema
EACM ilikuwa ni kampuni iliyoanzishwa kwa kuhusisha jiji na Mkurugenzi
wa Jiji la Dar es Salaam wakati huo alikuwa akiingia kwenye vikao akiwa
mjumbe.
Alisema awali, jiji na manispaa zake tatu lilibuni mradi
huo wa kujenga machinjio ya kisasa katika kiwanja chake cha Gongo la
Mboto kilichokuwa na thamani ya Sh bilioni moja ambacho kilitumika kama
sehemu ya mchango wa fedha katika hisa zake.
Alisema katika
mkataba huo, Manispaa za Ilala, Temeke na Kinondoni kila moja ilipaswa
kutoa Dola 500 za Marekani ikiwa ni mchango kwa hisa zake hivyo kufanya
tahamani ya mtaji kufikia Dola 2.5milioni.
“Lakini, kilichotokea ni
kwamba, fedha hizo za manispaa hazikutolewa katika kipindi ambacho mradi
ulipaswa kuanza. Hivyo, kampuni ikafilisika kwa sababu hata watu
wengine waliotaka kuwekeza fedha zao walisita baada ya kuona manispaa
hizo zinasuasua,” alisema.
Alisema kampuni iliyofanya upembuzi
yakinifu ilikuwa ya mhadhiri mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
(jina tunalihifadhi kwa kuwa hakupatikana kujibu madai hayo jana).
Simba
alisema hakuna fedha ambayo imeliwa na EACM kwani hata kiwanja hicho
ambacho ni mali ya halmashauri ya jiji, bado kiliachwa mikononi mwa
mamlaka hiyo.
Kuhusu ni kiasi gani cha fedha ambacho manispaa hizo
tatu zilitoa hadi kampuni hiyo ilipokuwa ikikaribia kufilisika, Simba
alijibu, “Sijui. Wewe umenikurupusha tu hapa sina nyaraka zozote.”
Lakini
alisisitiza kwamba EACM haikuwahi kuuza kiwanja hicho kwani bado
kiliachwa mikononi mwa jiji hilo hadi kampuni ilipofilisika.
|
No comments:
Post a Comment