Tuesday, March 27, 2012

Upinzani waingia Ikulu Senegal


RAIS wa Senegal Abdoulaye Wade (85), ameangushwa vibaya na mpinzani wake, Macky Sall (50) katika duru ya pili ya Uchaguzi Mkuu uliofanyika juzi.Matokeo hayo yamepokewa kwa hisia tofauti na wananchi wa Senegal na hata hapa nchini wengi wakisema anguko hilo la Wade ni somo kwa viongozi ving’ang’anizi wa madaraka barani Afrika.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana, wanasiasa, wasomi na wanaharakati nchini wamesema, anguko la Wade, linapaswa kuwa funzo kwa viongozi wanaokandamiza demokrasia katika nchi kadhaa barani Afrika.

Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (Tamwa), Ananilea Nkya alisema watawala wa Afrika wanapaswa kuheshimu uamuzi wa raia wanaotoa kupitia sanduku la kura.

“Wakati wa kuiba kura na kufanya hila nyingine ili mtu ashinde umepitwa na wakati. Kinachotakiwa ni kuheshimiwa kwa matakwa ya wananchi,” alisema na kuongeza: “Kilichotokea Senegal kinabainisha kuwa waliochaguliwa watakwenda kuwatumikia wananchi kwa kuwa hawakununua kura.”

Mbunge wa Wawi, Hamad Rashid alisema nchini kumekuwa na dhana kwamba upinzani una vurugu jambo ambalo alisema siyo la kweli isipokua hali hiyo inachangiwa na walio madarakani kutaka kuendelea kubaki hapo hata kama wananchi wanawakataa.

“Matokeo ya Senegal yanatufundisha kukubali kushindwa na kuwataka wanasiasa kuheshimu katiba,” alisema na kuongeza kuwa tume za uchaguzi zinapaswa kuacha demokrasia ikapata nafasi yake bila kuwafanya wengine kulazimika kutumia nguvu.

Mwenyekiti wa Tanzania Labour (TLP), Augustine Mrema alisema wananchi wamechoshwa na vyama vilivyokaa madarakani muda mrefu hivyo wanahitaji mabadiliko hata kama hayawapeleki wanapotaka.

Alisema watu wamechoshwa na vyama vya siasa vikongwe madarakani na wanapenda kuona mabadiliko hivyo ni wakati wa vyama vya namna hiyo ama kuachia ngazi au kuacha kura za wananchi zikaamua kwa kufuata misingi ya haki na demokrasia.

“Watu wamechoshwa na wapo tayari kwenda kwingine hata kama ni gizani,” alisema na kuongeza kuwa wale ambao wanahisi kuwa mfumo umewachoka ni vizuri wakakaa pembeni kwa heshima kuliko kusubiri kuondolewa kupitia masanduku ya kura.

Historia ya Wade

Kabla ya kuangushwa, Wade wa Chama Senegalese Democratic (PDS), tayari aliiongoza nchi hiyo kwa vipindi viwili mfufulizo tangu mwaka 2000 alipoingia madarakani na mwaka jana alibadili katiba ili aweze kugombea muhula wa tatu.

Senegal ambayo tayari ilikuwa ikinyemelewa na ghasia kutokana na Wade kubadili katiba, juzi ilipata Rais huyo mpya kutoka Chama cha Alliance for the Republic, baada ya kushinda kwa zaidi ya asilimia 60 huku mkongwe huyo akiambulia kiasi cha asilimia 30.

Awali, taarifa za Tume ya Taifa ya Uchaguzi Senegal zilisema  kulikuwa na jumla ya wapigakura zaidi ya milioni tano ambao waliandikishwa.

Ushindi huo wa Sall ambaye aliwahi kuwa mshirika kubwa kisiasa wa Wade ikiwa ni pamoja na kuwa Waziri Mkuu katika Serikali ya mkongwe huyo na Meneja wa kampeni iliyomuingiza madarakani kiongozi huyo mwaka 2000, umepokewa kwa nderemo na vifijo katika viunga vya jiji la Dakar na maeneo mengine nchini humo.

Hata hivyo, hadi jana jioni hakukuwa na taarifa rasmi za idadi ya wapigakura walioshirika katika duru hilo la pili la uchaguzi lililomng’oa Wade. Shirika la Habari la Serikali la Senegal (APS) lilitangaza kuwa Wade amekubali kushindwa na mpinzani wake huyo.

Kwa mujibu wa taarifa hizo, baada ya kutangazwa kwa matokeo hayo, Wade alimpigia simu mpizani wake Sall na kumwambia kuwa amekubali kushindwa. Taarifa hizo za APS zilisema Sall aliripotiwa kukubali kuzungumza mara tu baada ya mpinzani wake kukubali kuwa ameshindwa.

Kabla na baada ya duru ya pili

Katika duru ya kwanza, uchaguzi ulifanyika baada ya maandamano na vurugu katika kampeni za uchaguzi baada ya Wade kutumia mamlaka yake kutaka kuendelea kuwepo madarakani kwa kipindi kingine.

Wananchi hao walianza kujikusanya na kufanya maandamano kwa lengo la kumtoa Wade madarakani. Baada ya matokeo ya juzi, maelfu ya wafuasi wa Sall walijitokeza katika barabara za Dakar wakisherehekea ushindi wa kiongozi wao.

Miongoni mwa waliokuwa wakisherehekea ni Seynabou Seck ambaye alipohojiwa alisema: “Nimefurahi sana , Macky bado ni kijana na tena ni mtu mpole sana na ana heshima! Kwa hakika anastahili ushindi huu. Kila mtu alikuwa akimuombea ashinde.”

Akizungumzia ushindi wake, Sall alisema ni mwamko mpya kwa raia wa Senegal.
Katiba ya Senegal inaweka muda wa mihula miwili kwa rais kubaki madarakani na jaribio la Wade kuwania muhula wa tatu lilizusha maandamano na ghasia zilizosababisha vifo.

Wafuatiliaji wa kimataifa walisema uchaguzi huo ulifanyika kwa uhuru na amani ingawa polisi walirusha mabomu ya kutoa machozi nje ya kituo kimoja jijini Dakar.

No comments:

Post a Comment