Tuesday, March 27, 2012

Hesabu Mambo ya Ndani zawachefua wabunge

KAMATI ya Hesabu za Serikali Kuu (PAC), haikuridhishwa na hesabu za Wizara ya Mambo ya Ndani baada ya kubaini kuwapo upungufu uliosababisha kupata hati yenye mashaka kipindi cha miaka mitatu mfululizo.
Akizungumza kwenye kikao cha kamati hiyo Dar es Salaam jana, Kaimu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Ezekiah Chibulunje, alisema baada ya kamati kupitia vitabu vya wizara wamebaini kuwapo kwa matatizo kwenye hesabu na kusababisha baadhi ya fedha kutoonekana matumizi yake.

“Kamati haikuridhishwa na hesabu za wizara, hii ni mara ya kwanza kuona hesabu hazieleweki na wala hakuna kumbukumbu za kutosha tangu tulipoanza kupitia hesabu za wizara mbalimbali nchini,” alisema Chibulunje.

Alisema tatizo hilo linatokana na kuwapo kwa Mhasibu Mkuu mwenye elimu ya Diploma, ambayo imesababisha kushindwa kuweka kumbukumbu za matumizi ya fedha vizuri wakati Serikali inawataka wahasibu wakuu kuwa na elimu ya kiwango cha CPA.

Chibulunje alisema mhasibu huyo ameshindwa kutoa maelezo ya kueleweka kwenye kamati kuhusu matumizi ya fedha za Serikali na miradi ya wizara, jambo ambalo limesababisha kupata hati yenye mashaka kipindi chote.

Alisema kutokana na hali hiyo, kamati imeitaka wizara kukaa na wakaguzi kutoka Wizara ya Fedha na Uchumi kitengo cha hazina, ili kukagua hesabu zao na kutoa maelekezo ya upungufu uliojitokeza uweze kufanyiwa marekebisho.
Hata hivyo, Katibu mkuu wa wizara hiyo, Mbaraka Abdulwakil, alikiri kuwapo kwa upungufu huo na kudai kuwa, umetokana na mfumo wa mtandao uliosababisha baadhi ya hesabu kutoonekana.

Abdulwakil alisema wakati hazina imeanzisha mfumo mpya, walipata tatizo la kuziingiza fedha hizo jambo ambalo limesababisha baadhi ya fedha kutoonekana kwenye vitabu hivyo.

No comments:

Post a Comment