Tuesday, March 27, 2012

Wabunge waagiza jenereta kwa mkurugenzi wa Tanesco lizimwe

KAMATI ya Hesabu za Mashirika ya Umma(POAC), imeagiza Bodi ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kuondoa jenereta la dharura lililopo nyumbani kwa Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo, William Mhando kuanzia leo ili naye ajue machungu ya kukatika umeme mara kwa mara.

 Wakati POAC ikiagiza kuondolewa kwa jenereta hilo, taarifa zinaeleza kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Tanesco, Jenerali Mstaafu, Robert Mboma amemwandikia Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja akihoji sababu za kutokutekelezwa kwa agizo la Rais Jakaya Kikwete la kulipatia shirika hilo kiasi cha Sh408 bilioni kwa ajili ya kujiendesha.

Barua ya Mboma ya Machi 20, mwaka huu kwenda kwa Ngeleja, ambayo gazeti hili imefanikiwa kuiona, ilisema mnamo Machi, 8 mwaka huu, Rais Kikwete aliagiza Tanesco ipewe haraka mkopo huo wa Sh408 bilioni lakini akasema hadi sasa amri hiyo ya Amiri Jeshi Mkuu haijatimizwa.

“Mheshimiwa Rais tarehe 8 Machi aliagiza kuwa mkopo huo wa Sh408 bilioni upatikane haraka. Lakini, sisi tunazunguka na hivyo kushindwa kutii amri ya Amiri Jeshi Mkuu wa Tanzania. Katika hali ya kawaida, tunatakiwa tufanyekazi usiku na mchana kwa nia ya kukamilisha maagizo halali ya Rais wa Jamhuri ya Muungano," inasema sehemu ya barua hiyo ya Mboma.

Katika sehemu nyingine ya barua hiyo, Mboma alisisitiza: "Hali ya mabwawa yanayotegemewa ya Mtera na Nyumba ya Mungu ni mbaya sana. Ukosefu wa mafuta utatulazimu tutumie maji hayo... hii maana yake ni kuwa mwakani tutalazimika kukodi mitambo mingine ya dharura kwa sababu mitambo ya sasa, muda wake utakuwa umekwisha. Watanzania hawatatuelewa na Tanesco italaumiwa bure kwa sababu tuko ambao hatutii amri za ngazi za juu."

Mboma katika kuhakikisha agizo hilo la Rais linatekelezwa, aliomba kikao kati yake na Waziri Ngeleja, Katibu Mkuu wa Nishati na Madini, wajumbe wawili wa bodi, menejimenti ya shirika hilo na wajumbe wengine ambao waziri huyo angeona wanafaa.

“Lengo liwe ni kutafuta njia za kufanya ili turekebishe kasoro. Wakati huohuo; napendekeza Katibu Mkuu wetu azungumze na mwenzake wa Hazina. Hii iwe baada ya menejimenti ya Tanesco kumjulisha juu ya mazungumzo yao,” ilisisitiza barua hiyo na kuongeza:

“Itapendeza kama Katibu Mkuu (WNM) atakuwa amezungumza na mwenzake wa Hazina kabla ya kikao chetu. Baada ya hapo, naona tuone jinsi ya kuzungumza na mheshimiwa Rais. Suala hili ni zito."

Nakala ya barua hiyo ilipelekwa pia kwa Katibu Mkuu Kiongozi, Ofisi ya Rais, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Katibu Mkuu Nishati na Madini, Msajili Hazina na Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco.

Msimamo wa POAC

Mwenyekiti wa POAC, Zitto Kabwe akizungumzia suala la jenereta alisema ni lazima liondolewe kwa kuwa linatumia mafuta ya Serikali na ndiyo maana mkurugenzi huyo hawezi kujua adha iliyopo kwa wananchi pindi umeme unapokatika.

“Tumemtaka Jenerali Mboma afanye hivyo kwa kuwa haiwezekani mkurugenzi wa huyo awekewe jenereta kwani kwa kufanya hivyo inadhihirisha kwamba hawana umeme wa uhakika,” alisema.

Zitto alisema wameagiza hilo lifanyike haraka na kama mkurugenzi huyo anataka kuwa na jenereta anunue la kwake binafsi na si kutumia la umma na mafuta ya Serikali.

Alisema Tanesco imeendelea kuelemewa na mzigo wa kununua umeme kutoka makampuni binafsi na imepata hasara ya Sh47 bilioni kutoka Sh43 bilioni mwaka 2009.

Zitto alisemza mwaka 2010, Tanesco ilitumia kiasi cha Sh211 bilioni kununua umeme wa dharura kutoka kampuni binafsi na asilimia 90 ya fedha hizo zimetumika kwa Songas na IPTL… “Songas wametumia kiasi cha Sh127 bilioni na Sh64 bilioni zimetumika kwa IPTL.”
Alisema kutokana na hali hiyo wameitaka Tanesco kuanzia Mei mwaka huu, waache kutumia mitambo ya IPTL baada ya mtambo wao mpya wa Jacobsen unaojengwa Ubungo, Dar es Salaam kuanza kufanya kazi na kuzalisha megawati 100.

Zitto alisema hivi sasa Tanesco wamepunguza gharama za uendeshaji lakini wanatumia Sh499 bilioni kuzalisha na umeme ambao wakiuza wanapata Sh466 bilioni na ukiongeza gharama nyingine za mishahara unakuta wanapata hasara ya Sh47 bilioni kila mwaka.

Kuhusu kuwepo kwa mgawo wa umeme Zitto alisema Tanesco imekubali kuwa kuna mgawo usio rasmi na hiyo inatokana na kukosa dhamana kutoka serikalini ya kupata mkopo wa Sh408 bilioni ili iweze kununua umeme wa dharura na kuondokana na tatizo la umeme.

Zitto ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), alisema hali ndani ya shirika hilo ni mbaya kwa sababu haina fedha za kuliendesha na kwamba hawawezi kununua vipuri.

Alisema kutokana na hali hiyo umeme unaokatikakatika ni mgawo lakini shirika hilo limekuwa likikanusha kwa sababu uwezo limekuwa likipokea malalamiko mengi yanayohusu ukatikaji huo hasa Dar es Salaam.

“Hali ya mabwawa kwa mujibu wa taarifa ya Mwenyekiti wa Bodi ya Tanesco, Jenerali Mboma inaeleza kuwa ni mbaya kwani Mtera lina mita 1.24 tu juu ya kiwango cha chini kinachoruhusiwa na sasa bado mita 5.26 kufikia kima chake cha juu,” alisema Zitto na kuongeza:

“Nyumba ya Mungu ina mita 3.22 juu ya kina cha chini kinachoruhusiwa na ni mita 9.76 kufikia kina cha juu cha bwawa hilo hivyo maji kwenye mabwawa hayo ni kidogo hasa kama mvua haitanyesha maeneo ya Mbeya Dodoma, Arusha Kilimanjaro, Singida na Tanga.”

Alisema ukosefu wa fedha za kununulia mafuta utalazimu watumie maji hayo kidogo ili wasifanye mgawo wa umeme na hiyo maana yake ni kuwa mwakani watalazimika kukodi mitambo mingine ya dharura kwa sababu ya sasa muda wake utakuwa umekwisha.

Zitto alisema kutokana na hali hiyo, wamemwagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini kushughulikia suala hilo ili fedha hizo zipatikane.

“Mtambo wa Aggeko umezimwa na IPTL pia ambayo yote kwa ujumla huzalisha megawati 150,” alisema.

Awali, kabla ya kuhojiwa na POAC Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco, Mhandisi William Mhando alisema tatizo la umeme katika Mkoa wa Dar es Salaam litakwisha baada ya wiki nne kwa kuwa wahandisi wa shirika hilo wanafanyia kazi matatizo yaliyopo.Alisema kukatika umeme mara kwa mara hasa maeneo ya Mbagala, Temeke na Kigamboni kunatokana na mfumo wa umeme uliopo kuchakaa na ili kutatua tatizo hilo wameagiza transfoma nne za dharura.

“Hali ya umeme si mbaya tunamudu mahitaji kwa kutumia maji japokuwa si mengi na pia tunatumia gesi. Mifumo yetu ya umeme si mizuri kwa kuwa imechakaa,” alisema Mhando.

No comments:

Post a Comment