Tuesday, March 27, 2012

Mbowe: Kesheni kulinda kura

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe, ametangaza kuwa Aprili mosi ni siku ya mkesha wa kulinda kura kwa kila mwananchi mpenda demokrasia na maendeleo katika jimbo hilo.

 Akihutubia mikutano ya kumnadi mgombea wa chama hicho, Joshua Nassari, katika maeneo mbalimbali ya kata za Songoro, Ngarenanyuki, Leguruki, Nkoanrua na Maji ya Chai, Mbowe aliwataka wananchi wote wa jimbo hilo, hususan vijana, kukusanyika makao makuu ya Halmashauri ya Meru, ambako majumuisho ya mwisho ya kura yatafanyika kabla ya kutangaza matokeo.

“Ndugu zangu wana wa Arumeru Mashariki Aprili moja ambayo ni siku ya kupiga kura tumetangaza kuwa ni mkesha wa kulinda kura pale Halmashauri Usa River, wananchi wote, hasa vijana mkishapinga kura siku hiyo kwa amani kabisa, kwa utulivu, bila kumpiga wala kumsukuma mtu yeyote sindikizeni masanduku ya kura mpaka Usa River, tukifika pale tutasubiri matokeo pamoja ikibidi hata kukesha lakini hatutaondoka mpaka tumepata matokeo.

Mbowe alisema kuwa wamelazimika kufanya hivyo kwa kuwa Chama cha Mapinduzi na serikali yake wana mbinu nyingi za kuiba kura.

Akiwa katika kijiji cha Maruango, kata ya Leguruki, alisema kuwa uchaguzi wa Arumeru Mashariki si uwanja wa vita, akisisitiza kauli aliyoitoa wakati wa uzinduzi wa kampeni za chama hicho Machi 9, mwaka huu, kuwa CHADEMA itafanya mikutano ya amani na kistaarabu bila kumtukana mtu yeyote, huku akilitaka Jeshi la Polisi kuwa uwepo wake Arumeru kuwe ni sehemu ya matumaini na haki kutendeka, si kuibeba CCM na kuwatia hofu na woga wananchi.

Aliongeza kuwa utawala wa CCM umekuwa ukiwatisha watu badala ya kuwa sehemu ya matumaini na haki za wananchi, akionya kuwa hakuna utawala wa kidhalimu uliowahi kudumu milele, kwani CCM sasa badala ya kuwatia moyo wananchi na kuwapatia haki wamegeuka kuwatia hofu na kuwatisha, ikiwa ni ishara ya utawala wa kidhalimu.

“Ndugu zangu polisi ambao pamoja na kutupiga mabomu bado tunawatetea, nawaombeni sana muwe sehemu ya haki na matumaini ya wananchi hawa, fanyeni kazi yenu ya kulinda amani na usalama wa raia na mali zao, msifanye kazi ya kuibeba CCM, wala nguvu zenu hizo za kuibeba CCM hazitasaidia, uwepo wenu hapa usiwe kuwalinda mafisadi bali kulinda haki na matumaini ya watu hawa.

“CCM wanafanya vitendo vya kihalifu kwa watu wanaowapinga kifikra, kama hivi vya kumpiga mzee wa miaka sabini, wanapiga raia, tunataka polisi waliomwagwa hapa kwa wingi wachukue hatua dhidi ya wavunja sheria hao.

Aliongeza kuwa chama tawala kimeleta wabunge 50 na serikali imekwenda likizo kwa vile mawaziri wamehamia hapa huku Waziri wa Uratibu na Mahusiano, Stephen Wassira, akiongoza kampeni za matusi badala ya kutengeneza mahusiano.

“Mary Nagu naye anakuja hapa anatisha wajasiriamali kuwa wananchi wasipoichagua CCM watakiona, huyu ana pesa za wapi, serikali haina pesa zake, fedha zote ni mali ya umma. Kila Mtanzania anao uhuru na haki ya kujiunga na chama chochote anachokitaka. Tunasema hivi sisi tutawakosoa na kuwapinga kwa ajili ya maslahi ya wananchi,” alisema Mbowe.

Mzee wa CHADEMA apigwa na kijana wa CCM
Mzee mwenye umri wa miaka 65, Eliya Samweli, amedai kupigwa na kijana aliyemtaja kwa jina la Elibariki Karelia, kwa sababu ya uamuzi wake wa kujiunga na CHADEMA hivi karibuni na kukabidhiwa kadi ya chama hicho wiki iliyopita.

Akizungumza katika mkutano wa kampeni mbele ya Mbowe, Mzee Samweli alisema kuwa kijana huyo alimkuta akinywa soda madukani Maruango, akamtisha na kumnyang’anya simu na baadaye saa tatu kumvamia nyumbani kwake na kuanza kumpiga.

Alisema watoto wake walipiga yowe kuomba msaada wa majirani, ambapo mtuhumiwa alikimbia, huku akimtishia kuwa angemchomea moto nyumba yake.

CCM yamwaga matusi
Katika hali isiyo ya kawaida mkutano wa kampeni wa mgombea ubunge jimbo la Arumeru Mashariki kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi ( CCM ) Sioi Sumari ulitawaliwa na maneno ya matusi na vijembe dhidi ya viongozi wa CHADEMA.

Hali hiyo ilijitokeza jana wakati mgombea wa CCM , Sioi Sumari, alipokuwa akihutubia jukwaani aliporwa kipaza sauti na Meneja wa Kampeni hizo, Mwigulu Mchemba, ambaye alianza kumshambulia Katibu Mkuu wa CHADEMA , Dk. Willibrod Slaa kwa matusi akimwita kichaa.

Hatua hiyo ilitokana na kitendo cha helikopta ya CHADEMA kupita juu kwa mbali na ulipokuwa ukifanyika mkutano wa CCM, na kusababisha wananchi wengi waliokuwa kwenye mkutano huo kushangilia kwa kutumia salamu ya CHADEMA ya “Peoples Power” huku wakionyesha vidole viwili juu.

Hata hivyo ilibainika baadaye kuwa waliokuwa ndani ya ndege hiyo ni Mwenyekiti wa Taifa wa CHADEMA, Freeman Mbowe , mgombea wa CHADEMA, Nassari, na kiongozi wa kampeni hizo Vicent Nyerere ambao walikuwa wakielekea kwenye mkutano wao wa mwisho eneo la Maji ya Chai.

Naye mbunge wa Korogwe Vijijini Stephen Ngonyani aliwalalamikia makada wa CHADEMA kwa kumsakama kuwa ni mganga wa kienyeji wakati yeye ni muumini mzuri wa Kanisa la Anglikana.

NEC yawakoroga wapiga kura
UAMUZI wa Tume ya Uchaguzi wa kutaka kutuma taarifa za vituo vya kupigia kura kwa njia ya simu katika uchaguzi wa jimbo la Arumeru Mashariki umewakoroga baadhi ya wananchi, huku wengine wakiunga mkono.

NEC juzi ilisema kuwa sasa itawajulishwa wananchi vituo vyao vya kupigia kura kwa njia ya simu, jambo ambalo limezua zogo kwa baadhi ya maeneo. Wakiongea kwa nyakati tofauti jana baadhi ya wananchi wamekubaliana na utaratibu huo wakisema utawarahisishia na utawaondolea usumbufu usio na lazima wa kwenda kusimama muda mrefu kwenye vituo kutafuta majina yao.

“Utaratibu huu ni mzuri kwa sababu utatupunguzia usumbufu wa kwenda kusimama muda mrefu kwenye vituo vya kupigia kura tukitafuta majina,” alisema Jerome Kitomari.
Hata hivyo, wanaoupinga walisema kuna hatari ya kusababisha wapigakura wengi kukosa fursa ya kupiga kura pale itakapotokea mtu akapata maelekezo ya kituo lakini siku ya kupiga kura jina lake likakosekana.

“Huu utaratibu unaweza kuwa ‘changa la macho’ kwani tunaweza kutumiwa majina ya vituo kwenye simu lakini tukifika pale tukaambiwa majina hayaonekani kwenye orodha kwa siku hiyo sidhani kama itakuwa rahisi kupata msaada wa kujua jina lako liko kituo kipi hivyo ni dhahiri hautapiga kura,” alisema Salome Pallangyo.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Dk. Wilbroad Slaa alisema kuwa utaratibu huo ni mzuri kama ukitekelezwa ipasavyo lakini alitilia shaka kwa kile alichoeleza kuwa kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 ulitangazwa kuwa ungetumika lakini ulishindikana.

Msimamizi wa uchaguzi wa jimbo hilo, Trasias Kagenzi, mwishoni mwa wiki aliviandikia barua vyama nane vinavyoshiriki uchaguzi mdogo wa ubunge jimboni hapa akiwataka wawaelimishe wapiga kura namna ya kutumia ya simu za kiganjani kujua kituo cha kupiga kura .

Kwenye barua hiyo yenye kumbukumbu namba E . 50/9/2012/40 ya machi 24 , mwaka huu, Kagenzi alieleza kuwa kila mpiga kura atatakiwa kuandika namba yake kwenye kitambulisho chake kisha ataituma kwenda namba 15540 ambapo atatumiwa taarifa yake pamoja na kituo atakachotakiwa kupigia kura.

No comments:

Post a Comment