Tuesday, March 27, 2012

Tanesco hakueleweki

PAMOJA na Shirika la Umeme (Tanesco) kudai kuwa kukatikakatika kwa umeme kunakoendelea, kunatokana na shirika hilo kuzima mitambo ya Aggreko, taarifa ya uzalishaji wa umeme kwenye Gridi ya Taifa, imeonesha kuwa umeme unaozalishwa unatosha na kuzidi mahitaji.

Taarifa ya uzalishaji umeme kwa jana ambayo gazeti hili linayo, ilionesha kuwa umeme uliokuwa ukizalishwa katika Gridi ya Taifa bila kuwashwa kwa mitambo hiyo, ni megawati 742.60 wakati mahitaji halisi ya umeme ni Megawati 683.

Akifafanua hali hiyo ofisini kwake jana, Kamishna wa Nishati katika Wizara ya Nishati na Madini, Prosper Victus, alisema katizo la umeme la mara kwa mara linatokana na kuzeeka kwa mitambo ya kusambaza umeme ya Jiji la Dar es Salaam.

Wakati Victus akitoa taarifa hiyo, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Masharika ya Umma (POAC), Kabwe Zitto (Chadema), alidai kuwa Tanesco wamedai kuwa umeme unakatika kutokana na kuzimwa kwa mitambo ya Aggreko kulikosababishwa na kukosa fedha za kuendesha mitambo hiyo.

Zitto aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa shirika hilo limeshindwa kupata fedha za kuendesha mitambo ya Aggreko kutokana na Serikali kushindwa kutoa Sh bilioni 408 kwa Tanesco.

Fedha hizo ziliahidiwa kutolewa na Serikali ili kuisaidia kukabiliana na mpango wa dharura wa kuzalisha megawati 200 ambazo zinazalishwa kwa pamoja kati ya Aggreko na kampuni ya kufua umeme wa gesi ya Symbion. Kila kampuni inazalisha megawati 100.

“Tumeiagiza Serikali itoe fedha hizo ili kuepusha nchi kuingia kwenye mgawo mkubwa,” alisema Zitto ambaye katika kikao cha jana aliwazuia waandishi wa habari kushiriki kwenye majadiliano kati ya kamati na viongozi wa Tanesco.

Hata hivyo, Victus alifafanua kuwa mitambo hiyo imezimwa kwa kuwa hali ya uzalishaji wa umeme inaridhisha na umeme uliopo unapita mahitaji na mitambo iliyozimwa, ni kwa sababu ya akiba na itawashwa pale panapotokea ulazima wa kuiwasha.

Zitto alisema Kamati yake iliwahoji kwa kina maofisa wa Serikali wakiongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi kutaka kujua sababu ya kukatika mara kwa mara kwa umeme ambao walijitetea kuwa ni matatizo ya kiufundi.

“Lakini Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco (William Mhando) alipobanwa alisema tatizo hilo linatokana na kuzimwa kwa mashine za Aggreko,” alisema Zitto na kuongeza kuwa hadi jana Tanesco wanadaiwa zaidi ya Sh bilioni 230 na Aggreko.

Licha ya kuanza utekelezwaji wa mpango wa dharura, matatizo ya umeme bado yameendelea kuikumba nchi kutokana na kukatika mara kwa mara kwa nishati hiyo.

Jijini Dar es Salaam hasa maeneo ya katikati ya mji hali ni mbaya nyakati za mchana kutokana na maeneo hayo kukosa umeme kila siku mchana. Mwenyekiti huyo wa POAC alisema katika kupitia hesabu za Tanesco wamebaini kuwa shirika hilo liko taabani kifedha baada ya kupata hasara ya Sh bilioni 47 katika hesabu za mwaka 2010.

Akichambua hesabu hizo, Zitto alisema hasara hiyo inatokana na shirika hilo kutumia fedha nyingi kuyalipa makampuni ya Songas na IPTL ambayo yanaliuzia shirika hilo umeme.

Alitoa mfano kuwa mwaka 2010 Tanesco ilitumia Sh bilioni 211 kuilipa IPTL na Sh bilioni 126.9 kuilipa Songas kama malipo ya kununua umeme kutoka kwa kampuni hizo. “Suluhisho hapa ni kupunguza kununua umeme kwa IPTL ili shirika lipate faida…wakiachana na IPTL watapata faida,” alisema Zitto.

Alifafanua kuwa jumla Tanesco inatumai Sh bilioni 492.25 kama gharama za kununulia umeme wakati mapato yake ni Sh bilioni 466.77 kwa mwaka. Mbunge huyo alisema wameiagiza Tanesco kuhakikisha ifikapo Mei isitishe kununua umeme kutoka IPTL badala yake waharakishe kukamilisha mtambo wao wa kuzalisha megawati 100 unaosimikwa Ubungo.

Alisema Tanesco ikiachana na IPTL, itapata faida kwani IPTL inalinyonya shirika hilo fedha nyingi kuliko gharama za umeme wanaozalisha. Alisema licha ya mapato hayo, Tanesco inapokea Sh bilioni 106 kama ruzuku kutoka serikalini lakini shirika hilo linatumia fedha hizo kununua umeme pamoja na kulipa madeni hali inayolifanya lijikute limepata hasara hiyo ya Sh bilioni 47.

Wakati huo huo, kamati hiyo imemwamuru Mhando kung’oa jenereta analotumia na kulipiwa gharama na Tanesco. Uamuzi huo unatokana na madai kuwa Mkurugenzi huyo hapatwi na machungu ya mgawo wa umeme kwani jenereta hilo linatoa umeme muda wote mara tu ukikatika.

“Nimemwagiza Jenerali Mboma (Robert) ambaye ni Mwenyekiti wa Bodi ahakikishe jenereta hilo linang’olewa, la sivyo Mkurugenzi huyo ajigharimie mwenyewe mafuta na si kulipiwa na Tanesco,” alisema Zitto.

No comments:

Post a Comment