Tuesday, March 27, 2012

Mtei: Zitto haraka ya nini

MUASISI  wa Chadema, Edwin Mtei ameamua kuvunja ukimya na kuzungumzia kauli  ya mbunge Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe ya kutangaza nia ya kugombea urais mwaka 2015.

Amekosoa uamuzi wa mbunge huyo kwa madai kwamba amefanya mapema mno kutangaza nia yake.
Amesisitiza kwamba Chadema hawawezi kumchagua mtu aliyejitangaza mapema kuwania urais bali watatumia vigezo vya uadilifu na uwajibikaji kupitia vikao halali vya chama.
“Bado miaka mitatu,ni  mapema sana, hatuwezi kumchagua mtu aliyejitangaza mapema. Tutamchagua mtu kwa vigezo. Ni vizuri angesubiri vikao vya chama ndipo azungumze” alisema Mtei.

Mtei ambaye aliwahi kuwa Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) alivunja ukimya huo jana wakati akihojiwa na gazeti hili kuhusu kauli ya  Zitto inayoonekana kuwachanganya watendaji wakuu wa chama hicho.

Juzi, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe pamoja na Katibu Mkuu wake, Dk Willibrod Slaa walitoa maoni yao tofauti juu ya kauli hiyo ya Zitto.
Dk Slaa alikosoa hatua hiyo na kusema siyo wakati mwafaka sasa kuzungumzia urais, lakini Mbowe alisema hana tatizo na Zitto kutangaza nia hiyo kwa kuwa ni haki yake, lakini akahoji haraka ya kutangaza dhamira hiyo.

Hatahivyo,kwa nyakati tofauti viongozi hao walimshauri Zitto kufuata taratibu za chama kama anataka kufikia malengo yake hayo ya kutaka kuwania nafasi hiyo ya juu kabisa ya uongozi wa taifa.

Akihojiwa , Mtei alisema kwamba ni mapema sana kwa mwanachama wa Chadema kuelekeza akili yake ya kuwania urais kupitia chama hicho wakati muda bado haujafika.

Alisisitiza kwamba ni mapema sana kwa kuwa kuna watu ambao bado hata hawajaingia ndani ya Chadema na kujulikana kwa sasa hivyo alishauri wenye mawazo hayo kusubiri hadi muda uwadie.

Akizungumza kwa hisia muasisi huyo alibainisha ya kwamba kila mtu ndani ya Chadema ana msimamo wake lakini ni mapema sana mtu au kiongozi ndani ya chama hicho kuelekeza akili yake kuwania nafasi ya urais.

“Kila mtu ana msimamo wake ila tunasema ni mapema kusema mtu kuzungumzia nani atateuliwa na chama sasa ni mapema mno,”alisisitiza Mtei

No comments:

Post a Comment