Tuesday, March 27, 2012

Kanuni za kudhibiti misumeno ya moto zazinduliwa

WIZARA ya Kilimo na Maliasili imezindua kanuni ambazo zitadhibiti matumizi ya misumeno ya moto kwa ajili ya kukabiliana na kasi ya uharibifu wa mazingira inayotokana na ukataji wa miti uliokithiri.

Hatua hiyo imekuja baada ya kuwepo kwa wimbi la ukataji wa miti mbalimbali ikiwemo ya matunda kwa matumizi ya mbao na ujenzi kwa kutumia misumeno ya moto, zaidi vijijini Unguja na Pemba.

Akizindua kanuni hizo, Kaimu Waziri wa Kilimo na Maliasili Ramadhan Abdalla Shaaban alisema hivi sasa kuna kasi kubwa ya ukataji wa rasilimali za misitu kwa kiwango kinachotishia mazingira ya uhai wa miti.

Shaaban alisema kwa mwaka, hekta za misitu 950 zinakatwa bila ya kuzingatia suala zima la upandaji wa miti mipya kwa ajili ya matumizi mbalimbali.

Alisema Wizara imeamua kutunga kanuni mpya zitakazodhibiti matumizi mabaya ya ukataji wa misitu kutokana na kuwepo kwa misumeno ya moto.

“Zanzibar inakabiliwa na kiwango cha kutisha cha ukataji wa misitu usiozingatia uhifadhi wa mazingira, ndiyo maana tumetunga kanuni mpya za kudhibiti ukataji wa miti kutokana na kuwepo kwa matumizi ya misumeno ya moto,” alisema Shaaban.

Alisema kuanzia sasa mtu yeyote atakayemiliki msumeno wa moto, atalazimika kuomba maombi rasmi yatakayomhalalishia kumiliki msumeno huo baada ya kukubaliwa na idara husika ya ardhi.

Shaaban alisema adhabu kali itamkabili mtu atakayemiliki msumeno wa moto bila ya kibali husika ikiwemo kwenda chuo cha mafunzo jela miezi sita au kulipa faini Sh 300,000.

Viongozi waandamizi wa wizara hiyo wakifuatana na watendaji wa Idara ya Misitu walishiriki katika uchomaji moto misumeno iliyokamatwa na maofisa wa idara hiyo ambayo ilikuwa ikifanya kazi kinyume cha sheria kukata miti katika maeneo mbalimbali ikiwemo misitu ya Hifadhi ya Serikali.

Mapema Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini Unguja, Riziki Simai alikiri kuwepo kwa kasi ya ukataji wa miti ikiwemo minazi pamoja na miembe kwa matumizi ya mbao na ujenzi.

No comments:

Post a Comment