Tuesday, March 27, 2012

Wachungaji waonya viongozi serikalini

-Wasema hawana hofu ya Mungu, wakerwa na malumbano

VIONGOZI serikalini wameshauriwa kuacha kupoteza muda mwingi katika malumbano wakati Watanzania wakizidi kukabiliwa na hali ngumu ya maisha licha ya Taifa kuwa na rasilimali nyingi.
Mchungaji wa Huduma ya Hossana Alive Vision, Ephraim Mwansasu, aliyasema hayo Dar es Salaam jana wakati akizungumza kwa niaba ya wachungaji wenzake kwenye mkutano wa injili uliofanyika Mtoni Kijichi.

Alisema viongozi wengi serikalini, wanatumia muda mwingi kulumbana na wanasiasa waakati nchi inakabiliwa na changamoto nyingi.

“Umefika wakati wa wachungaji wote nchini kuungana ili kuliombea Taifa hili ambalo hivi sasa limepoteza mwelekeo kwa sababu ya uovu uliokithiri.

“Serikali iliyopo madarakani iangalie upya mwelekeo wa nchi yetu, kuacha malumbano na vyama vya siasa,” alisema Mchungaji Mwansasu na kuongeza kuwa, ipo haja ya Serikali kujipanga ili kuhakikisha inatatua matatizo yanayowakabili Watanzania.

Alisisitiza kuwa, Serikali ya Aawamu ya Nne ina viongozi wengi ambao hawana hofu ya Mungu moyoni mwao ndiyo maana kuna ufisadi mwingi.

Katika hatua nyingine Mchungaji Mwansasu aliwataka Wakristo kote nchini kumgeukia Mungu ili waweze kufanya mambo ya kumpendeza yeye na kufuata maagizo yake.

Alisema nyakati za sasa ni za mwisho ndiyo maana maasi yamekuwa mengi hivyo ni vyema Wakristo wakawa karibu na Mungu.

No comments:

Post a Comment