Tuesday, March 27, 2012

Kesi ya Kibanda, Makunga yapigwa kalenda

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Mwananchi Communication Ltd, Theophil Makunga, jana alipandishwa kizimbani na kusomewa mashtaka ya kuchapisha makala ya uchochezi yanayomkabili pia Mhariri Mtendaji wa Gazeti la Tanzania Daima, Absalom Kibanda, na mwandishi wa makala hiyo, Samson Mwigamba.

 Sambamba na hilo Wakili Mwandamizi wa Serikali Elizabeth Kaganda mbele ya Hakimu Mkazi Waliarwande Lema aliomba kufanya marekebisho ya ya majina ya washtakiwa wa pili na wa tatu (Kibanda na Makunga) ambayo Machi 7 yalikosewa kwa kuandikwa Kibamba, badala ya Kibanda na Maingu wakati jina halisi ni Makunga.

Wakili Kaganda akimsomea shtaka hilo ambalo kwa mujibu wa hati ya mashtaka ni la pili ambalo linamkabili Makunga peke yake ni kuchapisha waraka wa uchochezi kinyume na kifungu cha 32(1) ( c) na 31 (1)(a) vya Sheria ya Magazeti Na.229 kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.

Kwamba Novemba 30 mwaka 2011, Makunga akiwa na wadhifa huo alichapisha makala ya uchochezi iliyokuwa na kichwa cha habari kisemacho ‘ Waraka Maalum kwa Askari Wote’ ambayo iliandikwa na gazeti la Tanzania Daima Toleo Na. 2552 la Novemba 30 mwaka 2011.

Hata hivyo mshtakiwa alikana shtaka hilo na Hakimu Lema alisema masharti ya dhamana kuwa na wadhamini wawili ambao watasaini bondi ya sh milioni 5 kila mmoja, na kuwasilisha hati ya mali isiyohamishika yenye thamani hiyo ya fedha, kuripoti mara moja kwa mwezi katika Kituo Kikuu cha Polisi na kusalimisha hati ya kusafiria mahakamani, masharti ambayo yalitimizwa na Makunga na yuko nje kwa dhamana.

Wakili Kaganda pia aliikumbusha mahakama hiyo kuwa kesi hiyo jana ilikuwa imekuja kwa ajili ya upande wa jamhuri kuwasomea maelezo ya awali washtakiwa hao lakini hawakuwa tayari kwa jana na wakaiomba mahakama ipange tarehe nyingine ya kuwasomea maelezo hayo ya awali.

Hakimu Lema alikubaliana na ombi hilo na aliahirisha kesi hiyo hadi Aprili 24 kwa ajili ya washtakiwa kuja kusomewa maelezo ya awali.

No comments:

Post a Comment