Tuesday, March 27, 2012

Polisi akana Mahanga kukamatwa na masanduku ya kura

ALIYEKUWA Mkuu wa Kituo cha Polisi cha Buguruni, Mark Njela (37) ameieleza Mahakama kuwa hakupokea taarifa za aliyekuwa Mgombea wa Ubunge katika Jimbo la Segerea kupitia CCM, Dk Milton Mahanga kukamatwa na masanduku ya kura.

Aidha alidai kuwa hakuna matukio ya jinai yaliyotokea katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka juzi, likiwemo tukio la kuchomwa kwa Ofisi ya Mtendaji wa Kata ya Kiwalani iliyokuwa ikitumika kufanya majumuisho ya kura katika kata hiyo.

Njela, ambaye ni Mkuu wa Upelelezi wa Wilaya ya Kati ya kipolisi, alidai hayo jana katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam wakati akitoa ushahidi katika kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa jimbo hilo yaliyomtangaza Dk Mahanga kuwa mshindi.

Mwaka juzi mgombea ubunge wa jimbo hilo kupitia Chadema, Fred Mpendazoe alifungua kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa jimbo hilo dhidi ya Dk. Mahanga, Mwanasheria Mkuu wa Serikali na aliyekuwa msimamizi wa uchaguzi wa jimbo hilo kwa madai kuwa uchaguzi huo ulikiuka matakwa ya sheria ya uchaguzi ya mwaka 2010.

Akitoa ushahidi baada ya Wakili Seth Mkemwa kumuonesha gazeti la Mwananchi lililoripoti Dk Mahanga amekamatwa na masanduku ya kura katika eneo la Buguruni, Njela alidai alisikia taarifa hiyo na kuna mwandishi wa habari alimpigia simu lakini hakuna jalada lililofunguliwa.

“Hizi ni taarifa tu na ndio maana hata Kamanda wa Polisi Kanda ya Dar es Salaam, Suleiman Kova alijibu ofisi yake haina taarifa kwa sababu hakukuwa na tukio hilo na sisi ndio huwa tunampelekea taarifa hivyo na mimi najibu sina taarifa hizo,” alidai.

Wakili wa mdai, Peter Kibatala alimuuliza Njela kama amewahi kupokea taarifa zozote za matukio ya jinai zilizotokea katika kipindi cha uchaguzi, Njela alijibu hakupokea taarifa yeyote.

Alipoulizwa kuhusu tukio la kuchomwa kwa Ofisi ya Mtendaji wa Kata ya Kiwalani ambayo ilikuwa ikitumika kufanya majumuisho ya kura, Njela alidai alisikia lakini hakuthibitisha na tukio hilo halikuripotiwa katika kituo chake.

Kibatala alimuuliza Njela kama ni kweli Jeshi la polisi limekuwa likilalamikiwa sana na nchini kwa kutotenda haki na kuna ripoti nyingi zinaeleza jinsi polisi wanavyopendelea upande mmoja, Njela alijibu si kweli.

Alipoulizwa kama alipandishwa madaraka miezi saba baada ya uchaguzi, Njela alikiri kupandishwa madaraka kutoka Mkuu wa Kituo hadi kuwa Mkuu wa Upelelezi wa Wilaya ya Kati, huku akidai kupandishwa madaraka kulitokana na ufanisi wake wa kazi.

No comments:

Post a Comment