Friday, April 27, 2012

Mji wa Manchester kuwaka moto

Hatumwi mtoto dukani. Ni msemo uliowahi kuusikia mara nyingi, lakini siku ya jumatatu utakua sahihi.

Ni siku ambapo wababe wawili wa Ligi kuu ya Premier ya England watapambana ikiwa ni kwenye uwanja wa Etihad wa Manchester City.
Baina ya timu hizi zimefunga bao 173 katika Ligi msimu huu tukishuhudia mengi yaliyofungwa na Wayne Rooney, Sergio Aguero, Javier Hernandez na Carlos Tevez.
uwanja wa City

Majina haya yanakupa ufahamu kua kila upande unaweza kufanikiwa kuchota pointi kutoka uwanja wa Etihad na kwa ushindi apo Etihad pia Ligi ya msimu huu.
Ukitazama orodha ya majina utaingiwa na tamaa ya ya pambano la kuvutia kutokana na washambuliaji wenye mikwaju mikali bila kusahau wanaowalisha mipira ya kupasua nyavu.

Man.City kwa kipindi kirefu imemtegemea David Silva na bado anaweza kushawishi matokeo ya mechi wakati wowote huku United ikimtegemea mno Antonio Valencia aliyekua na ushawishi mkubwa msimu huu kwa kuvunja ngome nyingi za vilabu mbalimbali.
.
David Silva
Vijana wa Roberto Mancini walipoteza muelekeo baada ya siku kuu ya Krisimasi kipindi ambapo kiwango cha mcheza kiungo David Silva kilianza kushuka ingawa hivi sasa klabu yake imerejesha uwezo wa kufunga mabao kutokana na hali yake kua bora kwa sasa.

Na huku kurejea kwa mshtuko kwa Paul Scholes mwezi januari kunaweza kuonekana kama changamoto iliyoiwezesha United kupanda kilele cha Ligi kuu, ingawa mchango wa Valencia kutoka upande wa kulia ni mkubwa mno. Valencia.

Kufuatia jeraha la kisiginio la mda mrefu mapema msimu huu Valenzia alizinduka kwa kupachika wavuni bao mbili kati ya 4-1 dhidi ya Wolves tarehe 10 Disemba.
Kwa uchache, hawa ni wawili kati ya orodha ndefu ya wachezaji wa Manchester mbili zinazotambiana kushinda pambano la jumatatu litakaloamua mshindi wa Ligi ya mwaka huu.
Antonio Valencia
Tuangalie uwezekano wa hali inayoweza kujitokeza ikiwa kwa mfano:
City itashinda - basi timu hizi mbili zitakua sawa kwa pointi kukisalia mechi mbili, wingi wa goli za City ukiiweka klabu hio juu ya kilele.
Droo -na hapa United itahitaji pointi nne kutoka mechi zilizobaki, hata ikiwa City itashinda mechi zote zilizobaki.

Hapa ushindi wa United katika mechi itakayofuata dhidi ya Swansea basi itatangazwa United kua mshindi endapo City itashindwa kuifunga Newcastle ugenini.
Endapo United itashinda pambano la jumatatu basi Ligi itahesabu kombe la 20 la United.

Habari Mpya Jioni Hii: Kamati Kuu (CCM) yaridhia Kikwete Kulisuka Upya Baraza la Mawaziri


nape
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Kamati Kuu iliyokutana leo tarehe 27/04/2012  chini ya Mwenyekiti wake Mhe. Dr. Jakaya Mrisho Kikwete Jijini Dar es salaam, pamoja na mambo mengine imefanya yafuatayo.;

A. UTEUZI
Kamati Kuu imeteua wafuatao kuwa makaimu Katibu wa mikoa. Vituo vyao vya kazi vitapangwa baadae. Uteuzi huu unatokana na kuwepo kwa mikoa wazi mitano, mikoa hiyo ni;
Geita
Njombe
Simiyu
Katavi
Magharibi

Hivyo wafuatao wameteuliwa kuwa makaimu katibu wa CCM wa Mikoa.
1. Ndg. Hilda Kapaya
2. Ndg. Shaibu Akwilombe
3. Ndg. Hosea Mpangile
4. Ndg. Alphonce Kinamhala
5. Ndg. Aziz Ramadhani Mapuri

B. HALI YA KISIASA:
Rais amepokea taarifa na maazimio ya Kamati ya wabunge wa CCM na Kamati ya uongozi ya wabunge wa CCM juu ya kilichotokea kwenye bunge lililopita mjini Dodoma.
Taarifa hizo zimewasilishwa kwenye kamati kuu na kujadiliwa. Pamoja na taarifa hizo kamati Kuu imepokea taarifa ya jinsi Rais alivyojipanga kuchukua hatua za kuwawajibisha mawaziri na watendaji wa serikali na wale wa mashirika ya umma waliobainika kuhusika na ubadhirifu ulioinishwa na  taarifa ya Mkaguzi na mdhibiti mkuu wa hesabu za Serikali, Kamati za kudumu za bunge na wabunge bungeni.

Kamati Kuu imeamua yafuatayo;

1. Kamati Kuu inatambua na kuheshimu haki na wajibu wa wabunge kujadili utendaji wa serikali yao.Inapongeza juhudi za serikali kuhakikisha kuwa ripoti ya mkaguzi na mdhibiti mkuu wa hesabu za serikali inajadiliwa kwa uwazi na hivyo kuibua mapungufu yaliyojadiliwa.

2. Kamati Kuu imeridhika na imebariki uamuzi wa Rais  KULISUKA UPYA BARAZA LA MAWAZIRI na taasisi zingine zilizoanishwa katika ripoti hizo. Imesisitiza utekelezaji wa uamuzi huo ufanywe mapema iwezekanavyo.

Aidha kamati Kuu imeipongeza Kamati Teule ya baraza la wawakilishi Zanzibar iliyoundwa kuchunguza utendaji katika sekta mbalimbali kwenye serikali ya mapinduzi Zanzibar kwa taarifa yao.
Kamati Kuu inawapongeza wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kwa jinsi walivyojadili taarifa hiyo na pia Kamati Kuu inaipongeza Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa kuipokea taarifa na kuanza kuifanyia kazi.


Nape Moses Nnauye
Chama Cha Mapinduzi
The Ideology and Publicity Secretary

Tuesday, April 24, 2012

BREAKING NUUUUUUUZ: HALI NI TETE BAHARI YA HINDI NJE KIDOGO NA NUNGWI ZANZIBAR KUNA SEMEKANA MAWIMBI MAKUBWA YA TORNADO'S YATUA ENEO MASAA MACHACHE YALIYO PITA



 Mawimbi yakiwa yanakuja kwa kasi ya ajabu katika Eneo La Nungwi Muda mchache ulio pita
Mawimbi yakizidi kusogea Eneo La Nungwi 

****
Taarifa za awali zinasema kwamba Mawimbi hayo makali sana yalisogea eneo la Nungwi lakini mpaka sasa hakuna Hatari yoyote imetajwa... Endelea kufuatilia

NAMNA YA KUPIKA CHAPATI ZA MAJI/ MAYAI

Mahitaji:
Unga wa ngano 500g
Mayai 2
Sukari tablespoon 3
Chumvi teaspoon 1/2
Kitunguu  1/2         (kata vipande vidogo vidogo sana)
Hiliki 1/4 teaspoon (iliosagwa ikawa unga)
Siagi (kama Blueband au inayofanania na hiyo)

Hatua ya kwanza unapasua mayai, kisha unayakoroga katika chombo chenye nafasi ya kutosha.


Unaweka kitunguu mara tu baada ya mayai
 
Unaweka chumvi na sukari unaendelea kukoroga
Huku ukiweka unga wa ngano kidogo, kidogo
Na unakuwa unaongeza na maji taratibu
Huku ukiangalia uzito wa uji
Usiwe mzito sana, wala mwepesi sana
Piga piga mpaka uhakikishe mabonge bonge yote yamekwisha
Weka hiliki koroga tena
Baada ya hapo utakuwa umepata mchanganyiko wa kutengenezea Pancakes.
Weka kikaango katika moto wa wastani
Majiko yanatofautiana settings
Kwahiyo basi, kutokana na jiko lako moto uwe wa kati

Jinsi ya kuzipika:
Unaweka siagi kwenye kiaango
Unamimina unga unaacha mpk ukauke
Kabla ya kugeuza upande wa pili unapaka tena siagi
Pancake haichomwi zaidi ya dakika 3

Kwa kipimo hicho unaweza kupata Pancake 20-25
Ukitaka pungufu unakata vipimo nilivyoelezea nusu yake
Ambapo unaweza kupata Pancakes 10-12

Unasukumia na mboga yoyote unayoipenda yenye sause ya kuchovyea. Na raha yake uzile kwa mkono msafi.

Monday, April 23, 2012

Jitu zima laishi kama mtoto





Mwanaume mmoja (Jitu zima) nchini Marekani mwenye umri wa miaka 31, amekuwa akiishi kama mtoto mchanga kwa muda wa miaka 18 iliyopita huku akivaa nepi, kunyonya vidole na kucheza michezo yote ya watoto wa miaka miwili.



Pamoja na kutimiza miaka 31, Stanley Thornton huku akiwa na umbile kubwa na uzito wa kilo 133 na urefu wa mita 1.67 bado anaendelea kuigiza maisha ya kitoto ambayo anayafurahia.
Akiongea na gazeti moja la nchini kwao, Stanley alisema kuwa anafurahia sana maisha hayo na haoni sababu ya kuwa mwanaume mkubwa kutokana na umri wake.


Stanley analishwa kama mtoto mchanga ambapo amekuwa akiwaajiri wanawake mbalimbali kumhudumia kama mama yake, wakimlisha chakula kwa kijiko, kumuimbia na kumfanyia kila anachostahili mtoto kufanyiwa.
Cha kushangaza Stanley ana fedha za kuwaajili akina mama, anazozipata kutoka serikalini ambako ana shughuli maalumu ambayo haikutajwa. Hivi karibuni Stanley alijitangaza katika televisheni kuwa anatafuta mama atakayekaa naye muda wote.

Spika aitupa ripoti ya Jairo

Aeleza ugumu wa utekelezaji wa kanuni ya 94

SPIKA wa Bunge, Anne Makinda, amesema hajaridishwa na majibu ya serikali kuhusu taarifa ya utekelezaji wa maazimio ya kamati ya Bunge kuhusu sakata la aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, David Jairo, hivyo kuirudisha serikalini.

Spika Makinda alitoa kauli hiyo jana, baada ya Mbunge wa Karatu, Mchungaji Israel Natse, kutaka mwongozo wa Spika katika suala hilo kutojadiliwa huku mkutano wa Bunge ukiwa unaahirishwa.

“Mheshimiwa Spika naomba kupata mwongozo wako katika order paper inaonekana Bunge linaahirishwa leo, lakini hakuna taarifa ya serikali kuhusu utekekezaji wa maazimio ya kamati ya Bunge kuhusu suala la Jairo na mpaka sasa hatujaambiwa chochote,” alisema.

Akijibu Spika Makinda alisema, “Tulikuwa tuweke katika mkutano huu, lakini mimi nimeyakataa majibu kwa kuwa sijaridhishwa, hivyo nimerudisha serikalini,” alisema Spika.
Jairo, alisimamishwa kazi kutokana na sakata la kuzichangisha fedha taasisi zilizokuwa chini ya wizara hiyo kwa lengo la kufanikisha kupitisha bajeti bungeni.

Kutokana na hali hiyo, Bunge liliunda Kamati Teule ya Bunge iliyoongozwa na Mbunge wa Tunduru Kaskazini, Ramo Makani, kuchunguza uhalali wa utaratibu wa wizara hiyo kuchangisha fedha hizo na kubaini kasoro kadhaa kabla ya kutoa mapendekezo yake.

Kamati hiyo iliundwa baada ya kuibuka mvutano baina ya mihimili miwili ya dola, Bunge na Serikali baada ya aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo, kutangaza hadharani kumrejesha kazini Jairo aliyekuwa amesimamishwa kazi kwa tuhuma hizo zilizotolewa bungeni dhidi yake.

Hata hivyo, siku chache baada ya wabunge kuja juu kupinga uamuzi huo wa Luhanjo, Ikulu ilitangaza rasmi kushughulikia tuhuma za rushwa zinazomkabili Jairo, baada ya Rais kumpa likizo yenye malipo na alipofanya uteuzi wa makatibu wakuu alimwacha pembeni na nafasi hiyo akampa Eliakimu Maswi.

Wakati huohuo, Spika wa Bunge alisema leo wabunge wamelazimika kujadili kamati ya mipango baada ya kuahirishwa kwa Bunge kutokana na kubanwa na kanuni ya 94.
Alisema kutokana na hali hiyo, kuna haja ya kuiangalia upya kanuni hiyo, hivyo mjadala wa kamati hiyo utafanyika katika ukumbi wa Msekwa.

“Kanuni ya 94 imekuwa na ugumu katika utekelezaji, hivyo kamati ya uongozi imeamua mjadala wa mpango wa maendeleo ya taifa kwa mwaka 20012/2013 ufanyike kesho (leo) katika ukumbi wa Msekwa, ili Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na maofisa wengine waweze kushiriki katika mjadala huo na kutoa majibu kwa hoja zitakazoibuliwa na wabunge,” alisema.

CHADEMA yaishukia Ikulu

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimeishambulia Ofisi ya Rais Ikulu juu ya kauli yake kwamba Rais Jakaya Kikwete alikuwa hajakutana na Waziri Mkuu Mizengo Pinda kumjulisha kile kilichotokea bungeni wiki jana, kinadhihirisha ombwe kubwa la uongozi katika ofisi ya Rais na udhaifu wa kiuongozi wa Rais na serikali kwa ujumla.

Taarifa ya CHADEMA iliyotolewa na Mkurugenzi wa Habari na Uenezi, John Mnyika, ilisema kuwa Ikulu imeonyesha bayana kuwa Rais Kikwete ni mzito wa kuchukua hatua kwa kuwa masuala ambayo yamezuka bungeni anayafahamu kwa kuwa yamepitia kwenye Baraza la Mawaziri ambalo yeye analiongoza na pia yapo kwenye taarifa mbalimbali ambazo mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali amemkabidhi nakala kwa nyakati mbalimbali.

Aidha CHADEMA imesema taarifa hiyo ya Ikulu imedhihirisha namna ambavyo safari za mara kwa mara za Rais zinavyolifanya taifa likose uongozi wake katika masuala ya msingi yanayoikabili nchi; hivyo ni muhimu asitishe safari ili kupunguza matumizi ya fedha wakati huu ambapo serikali ina ufisadi na matumizi makubwa hatua ambayo itamwezesha kubaki nchini kushughulikia masuala muhimu yanayolikabili taifa.

Kwa upande mwingine, CHADEMA imesema taarifa hiyo ya Ikulu iliyokuwa ikikanusha habari zilizoandikwa na Tanzania Daima juzi, inadhihirisha kwamba hakuna mawasiliano ya karibu na ya mara kwa baina ya Rais Kikwete na Waziri Mkuu Pinda wakati kwa mujibu wa ibara ya 52(3) na 53 (1) Waziri Mkuu ndiye msimamizi wa utekelezaji wa maagizo ya Rais anayewajibika kwa Rais.
“Hali hii imekuwa ikijirudiarudia katika matukio kadhaa kwenye kipindi cha kati ya mwaka 2008 mpaka 2011; ikiwemo matukio ya kashfa ya aliyekuwa Katibu Mkuu wa Nishati na Madini, David Jairo.

“Baraza hili la mawaziri kuendelea mpaka sasa kwa hali hii ni ishara ya udhaifu wa mamlaka ya uteuzi ambayo ni Rais Kikwete kwa kuwa ibara ya 57 (1) (c) ya Katiba imempa madaraka kufuta uteuzi na kuwaondoa madarakani mawaziri; hivyo Rais Kikwete athibitishe kwa matendo badala ya maneno matupu kuwa hawalindi mawaziri kwa kuwafukuza waliotajwa kwa kukiuka sheria,” ilisema taarifa ya CHADEMA.

Juzi Ikulu ilikanusha habari kuwa Rais alikuwa amewasiliana na Waziri Mkuu Pinda kuhusiana na suala la kujiuzulu kwa mawaziri, ikidai kuwa tangu awasili kutoka Brazil, Kikwete alikuwa hajakutana wala kuzungumzia suala hilo na waziri wake.

HOTUBA YA MHESHIMIWA MIZENGO P. PINDA (MB), WAZIRI MKUU WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA WAKATI WA KUAHIRISHA MKUTANO WA SABA WA BUNGE LA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA – DODOMA, TAREHE 23 APRILI 2012


UTANGULIZI

Mheshimiwa Spika,
1. Nitumie nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa Rehema kwa kutuwezesha kutekeleza majukumu yote yaliyopangwa kwa ufanisi mkubwa katika Mkutano huu wa Saba wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ulioanza tarehe 10 Aprili 2012. Tumefanikiwa kufanya hivyo kutokana na maandalizi mazuri ya Mkutano, ushirikiano miongoni Mwetu na Waheshimiwa Wabunge wote kujiandaa vizuri katika kuchangia hoja mbalimbali zilizopangwa.

Mheshimiwa Spika,
2. Katika Mkutano huu, tumepata Waheshimiwa Wabunge Wapya Wawili wote kutoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA). Napenda kutumia nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Joshua Samwel Nassari kwa kuchaguliwa kuwa Mbunge Mpya wa Jimbo la Arumeru Mashariki. Vilevile, nampongeza Mheshimiwa Cecilia Daniel Paressokwa kuteuliwa kuwa Mbunge kupitia Viti Maalum (CHADEMA). Kipekee kabisa nawapongeza Wananchi wa Arumeru Mashariki kwa kutumia haki yao ya Kidemokrasia vizuri. Lakini kwa dhati kabisa, nakipongeza Chama Cha Mapinduzi kwa kukubali Matokeo ya Uchaguzi Mdogo wa Arumeru Mashariki. Kitendo hicho kinaonesha uungwana na ukomavu wa Kisiasa na Demokrasia katika Nchi yetu. Huu ni mfano mzuri wa kuigwa na Vyama vingine vyote vya Siasa Nchini.

3. Kwa Waheshimiwa Wabunge wapya tunawatakia mafanikio na tunawaahidi ushirikiano wetu ndani ya Bunge na katika Kujenga Taifa letu. Vilevile, napenda kutumia nafasi hii pia kuwapongeza Waheshimiwa Madiwani wote waliopata Ushindi katika Chaguzi zilizofanyika katika Kata za Vijibweni (Temeke), Kiwangwa (Bagamoyo), Kirumba (Mwanza), Logangabilili (Bariadi), Chang’ombe (Dodoma), Kiwira (Rungwe), Lizaboni (Songea) na Msambweni (Tanga). Tunawatakia wote waliochaguliwa afya njema na maisha mazuri ili muweze kuwatumikia Wananchi waliowachagua na Taifa kwa ujumla.