UTANGULIZI
Mheshimiwa Spika,
1. Nitumie nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa Rehema kwa kutuwezesha kutekeleza majukumu yote yaliyopangwa kwa ufanisi mkubwa katika Mkutano huu wa Saba wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ulioanza tarehe 10 Aprili 2012. Tumefanikiwa kufanya hivyo kutokana na maandalizi mazuri ya Mkutano, ushirikiano miongoni Mwetu na Waheshimiwa Wabunge wote kujiandaa vizuri katika kuchangia hoja mbalimbali zilizopangwa.
Mheshimiwa Spika,
2. Katika Mkutano huu, tumepata Waheshimiwa Wabunge Wapya Wawili wote kutoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA). Napenda kutumia nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Joshua Samwel Nassari kwa kuchaguliwa kuwa Mbunge Mpya wa Jimbo la Arumeru Mashariki. Vilevile, nampongeza Mheshimiwa Cecilia Daniel Paressokwa kuteuliwa kuwa Mbunge kupitia Viti Maalum (CHADEMA). Kipekee kabisa nawapongeza Wananchi wa Arumeru Mashariki kwa kutumia haki yao ya Kidemokrasia vizuri. Lakini kwa dhati kabisa, nakipongeza Chama Cha Mapinduzi kwa kukubali Matokeo ya Uchaguzi Mdogo wa Arumeru Mashariki. Kitendo hicho kinaonesha uungwana na ukomavu wa Kisiasa na Demokrasia katika Nchi yetu. Huu ni mfano mzuri wa kuigwa na Vyama vingine vyote vya Siasa Nchini.
3. Kwa Waheshimiwa Wabunge wapya tunawatakia mafanikio na tunawaahidi ushirikiano wetu ndani ya Bunge na katika Kujenga Taifa letu. Vilevile, napenda kutumia nafasi hii pia kuwapongeza Waheshimiwa Madiwani wote waliopata Ushindi katika Chaguzi zilizofanyika katika Kata za Vijibweni (Temeke), Kiwangwa (Bagamoyo), Kirumba (Mwanza), Logangabilili (Bariadi), Chang’ombe (Dodoma), Kiwira (Rungwe), Lizaboni (Songea) na Msambweni (Tanga). Tunawatakia wote waliochaguliwa afya njema na maisha mazuri ili muweze kuwatumikia Wananchi waliowachagua na Taifa kwa ujumla.
Mheshimiwa Spika,
4. Katika Mkutano huu wa Saba wa Bunge tulifanya Uchaguzi wa Wawakilishi wa Nchi yetu katika Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki. Napenda nitumie nafasi hii kuwapongeza wafuatao kwa kuchaguliwa kuwa Wabunge wa Bunge hilo, Mheshimiwa Makongoro Nyerere; Mheshimiwa Abdullah Hassan Mwinyi; Mheshimiwa Nderakindo Kessy; Mheshimiwa Angela Kizigha; Mheshimiwa Adam Kimbisa; Mheshimiwa Twaha Issa Taslima; Mheshimiwa Bernard Murunya; Mheshimiwa Shy-Rose Bhanji; na Mheshimiwa Mariam Ussi Yahya. Tunawapongeza Wote! Tuna imani kubwa kwamba watatuwakilisha vyema katika Bunge la Jumuiya ya Afrika ya Mashariki kwa maslahi ya Tanzania Kiuchumi na Kijamii na Nchi zote kwa ujumla.
Mheshimiwa Spika,
5. Tangu kuhitimishwa kwa Mkutano wa Sita wa Bunge lako Tukufu, kumekuwepo na matukio mbalimbali ya kusikitisha, kusononesha, kuhuzunisha na yenye Majonzi makubwa yaliyosababishwa na Misiba na Ajali ambazo zimesababisha Vifo na kujeruhi Watanzania wenzetu wakiwemo Waheshimiwa Wabunge.
6. Napenda kupitia Bunge lako Tukufu, kutoa Salaam za Rambirambi kwa Familia, Ndugu, Jamaa na Marafiki wa Watanzania wote waliopoteza Maisha. Tuwaombee Marehemu wote ili Mwenyezi Mungu azilaze Roho zao Mahali Pema Peponi. Amina!
7. Vilevile, nawapa pole Majeruhi wote walionusurika na kupata Majeraha kutokana na Ajali mbalimbali zikiwemo ajali za Magari, Pikipiki, Baiskeli na vifaa vingine vya barabarani na ile ya Shirika la Ndege Nchini (ATCL) iliyotokea kule Kigoma.
Mheshimiwa Spika,
8. Wote tunafahamu kwamba katika kipindi hiki tumekuwa na Waheshimiwa Wabunge wenzetu ambao wamekuwa wakisumbuliwa na Maradhi mbalimbali. Tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kusikia Maombi yetu. Wote tumefarijika kutokana na kurejea kwa Mheshimiwa Dkt. Harrison George Mwakyembe ndani ya Bunge lako Tukufu akiwa na Afya Njema. Tunaamini Afya yake itazidi kuimarika katika siku zijazo. Vilevile, ni matumaini yetu makubwa kwamba, wenzetu wengine akiwemo Mheshimiwa Profesa Mark James Mwandosya, Mbunge wa Jimbo la Rungwe Mashariki na Waziri wa Maji; Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, Mbunge wa Chato na Waziri wa Ujenzi; pamoja na Mheshimiwa Highness Samson Kiwia, Mbunge wa Ilemela ambao bado wako katika Matibabu watapata nafuu haraka itakayowawezesha kuungana na sisi tena ndani ya Bunge letu Tukufu.
Mheshimiwa Spika,
9. Mwisho, naungana na Watanzania wote kuipongeza Timu ya Simba kwa kufikia Mzunguko wa Tatu wa Mashindano ya Kombe la Mabingwa Barani Afrika. Sote tunawatakia Maandalizi mema ili wazidi kufanya vizuri katika Mechi zijazo kwa kuwa ushindi wao ni ushindi wa Nchi yetu. Kwa Wachezaji na Viongozi, wao nawaasa msibweteke na ushindi mlioupata, ila mnatakiwa kuelewa kuwa safari bado ni ngumu na ndefu.
SHUGHULI ZA SERIKALI
(a) Maswali
Mheshimiwa Spika,
10. Katika Mkutano huu wa Saba tunaouhitimisha leo, Jumla ya Maswali 131 ya Msingi na mengine 315ya Nyongeza kutoka kwa Waheshimiwa Wabunge yalipata majibu ya Serikali. Vilevile, jumla ya Maswali 16 ya Msingi na 9 ya Nyongeza kupitia utaratibu wa Maswali ya Papo kwa Papo kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu yalijibiwa.
(b) Miswada
Mheshimiwa Spika,
11. Katika Mkutano huu Miswada ifuatayo ilisomwa na kujadiliwa:
(i) Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali za Biashara wa Mwaka 2011 [The Business Laws (Miscellaneous Amendments) Bill, 2011];
(ii) Muswada wa Sheria ya Taasisi ya Utafiti wa Mifugo Tanzania wa Mwaka 2011 (The Tanzania Livestock Research Institute Bill, 2011);
(iii) Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria za Mifuko ya Hifadhi ya Jamii wa Mwaka 2012 [The Social Security Laws (Amendments) Act, 2012]; na
(iv) Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali wa Mwaka 2011 [The Written Laws (Miscellaneous Amendments) (No.2) Act, 2011].
Vilevile, Muswada wa Sheria ya Haki za Wagunduzi wa Mbegu za Mimea wa Mwaka 2012 [The Plant Breeder’s Rights Bill, 2012] ulisomwa kwa mara ya kwanza.
(c) Taarifa Mbalimbali
Mheshimiwa Spika,
12. Bunge lako Tukufu lilipata fursa ya kupokea na kujadili Taarifa mbalimbali kama ifuatavyo:
(i) Taarifa za Kamati za Bunge zinazosimamia Fedha za Umma; na
(ii) Taarifa za Kamati za Bunge za Kisekta na zisizo za Kisekta.
Mheshimiwa Spika,13. Napenda nitumie nafasi hii kuwashukuru kwa dhati Waheshimiwa Wabunge wote kwa kazi nzuri ambayo wameifanya katika siku zote za Mkutano huu zikiwemo kujadili na kupitisha Miswada niliyotaja hapo juu. Nawashukuru pia kwa michango yenu wakati wa kujadili Taarifa mbalimbali zilizowasilishwa hapa Bungeni.
Mheshimiwa Spika,
14. Kipekee kabisa nitumie nafasi hii kuwapongeza Wenyeviti na Wajumbe wa Kamati za Bunge zilizowasilisha Taarifa mbalimbali mbele ya Bunge lako Tukufu. Ni dhahiri kuwa utaratibu huu unatoa fursa kwa Waheshimiwa Wabunge kupitia kwa kina masuala mbalimbali ya Kisekta na kutoa ushauri kwa Serikali. Aidha, utaratibu huu unatusaidia kuwepo kwa ‘Checks and Balances’ ndani ya Nchi yetu. Niwashukuru pia Wabunge wote kwa jinsi walivyochangia kwenye mjadala wa kujadili Taarifa hizo.
Waheshimiwa Wabunge wameonesha hisia zao katika kujadili masuala yote haya muhimu na mengineyo na hasa katika Mwenendo wa Matumizi ya Fedha za Serikali kwenye Wizara, Taasisi za Umma, Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa. Nawashukuru sana kwa kujadili Taarifa zote kwa uwazi na hatimaye kutoa mapendekezo kwa Serikali namna ya kushughulikia matatizo yaliyojitokeza kwenye maeneo mbalimbali.
Mheshimiwa Spika,
15. Mapendekezo ya Waheshimiwa Wabunge yako katika makundi muhimu yafuatayo:
Kwanza: Ni uimarishaji wa Uongozi na Utendaji katika Wizara, Taasisi za Serikali, Mashirika ya Umma, Mikoa na Serikali za Mitaa;
Pili: Ni usimamizi wa Sheria, Kanuni na Taratibu zinazohusu masuala ya Mapato na Matumizi ya Fedha;
Tatu: Ni uimarishaji wa hatua za Kupambana na Rushwa, Ubadhirifu na Wizi wa Mali za Umma;
Nne: Ni uendelezaji wa hatua za kubana matumizi yasiyo ya lazima ndani ya Serikali na Vyombo vyake; na
Tano: Ni ulinzi wa Rasilimali za Nchi kwa maslahi ya Taifa letu.
Mheshimiwa Spika,
16. Siku zote Serikali imekuwa tayari kupokea ushauri wa Bunge lako Tukufu na baada ya kusikiliza mjadala na mapendekezo ya Waheshimiwa Wabunge, Serikali inaahidi kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa Ushauri na Mapendekezo yaliyomo katika Taarifa hizo. Niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwamba Serikali itachukua hatua stahiki kuimarisha usimamizi na utendaji ndani ya Wizara na Serikali za Mitaa na Vyombo vyake na kuhakikisha Viongozi na Watendaji wake wanafanya kazi kwa umakini na uadilifu zaidi.
Mheshimiwa Spika
17. Katika Hotuba yangu hii ningependa kuzungumzia kwa kifupi mambo machache yanayohusu: Hatua zilizofikiwa katika Mchakato wa Kutekeleza Sheria ya Mabadiliko ya Katiba; Dhana ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii; Matokeo ya Shule za Msingi na Kidato cha Nne Mwaka 2011; Maendeleo ya Viwanda; Sensa ya Watu na Makazi; na mwisho Mpango wa Kutoa Kifuta Machozi cha Mifugo.
HATUA ZILIZOFIKIWA KATIKA MCHAKATO WA KUTEKELEZA SHERIA YA MABADILIKO YA KATIBA
Mheshimiwa Spika,
18. Kama Waheshimiwa Wabunge watakavyokumbuka, katika Mkutano wa Sita mwezi Februari 2012, Bunge lako Tukufu lilijadili na kupitisha Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba (Sura ya 83). Napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kuwa, mara baada ya Marekebisho hayo kupitishwa, Mheshimiwa Rais Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete kupitia Tangazo la Serikali Namba 66 la tarehe 24 Februari 2012; alialika Vyama vya Siasa vyenye Usajili wa Kudumu, Jumuiya za Dini, Asasi za Kiraia, Taasisi na Makundi ya Watu wenye malengo yanayofanana kuwasilisha kwake majina ya watu wanaoweza kuteuliwa kuwa Wajumbe wa Tume itakayoratibu na kukusanya maoni ya Wananchi kuhusu Mabadiliko ya Katiba.
19. Kwa mujibu wa Tangazo hilo, siku ya mwisho ya kuwasilisha mapendekezo ya majina ilikuwa tarehe 16 Machi 2012. Hata hivyo, kutokana na umuhimu wa zoezi hilo na ili kutoa fursa zaidi kwa Wananchi na Taasisi au Makundi yaliyopo Mikoani, Mheshimiwa Rais kupitia Tangazo la Serikali Namba 101 la tarehe 16 Machi 2012 aliongeza muda huo hadi tarehe 23 Machi 2012. Mapendekezo ya majina yaliyopokelewa yalikuwa mengi na hivyo kumpa Mheshimiwa Rais uwanja mpana zaidi wa kufanya uteuzi.
Mheshimiwa Spika,
20. Tarehe 6 Aprili 2012, Mheshimiwa Rais baada ya kushauriana na Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, aliteua Wajumbe 32 wa Tume itakayoratibu na Kukusanya Maoni ya Wananchi kuhusu Mabadiliko ya Katiba. Pamoja na Wajumbe hao, Mheshimiwa Rais aliteua Katibu na Naibu Katibu wa Tume hiyo. Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti, Wajumbe, Katibu na Naibu Katibu wa Tume waliapishwa na Mheshimiwa Rais tarehe 13 Aprili 2012. Kutokana na umuhimu wa Tume hii katika historia ya Nchi yetu, naomba niwataje Wajumbe wote wa Tume walioteuliwa:
1. Mheshimiwa Jaji Joseph Sinde WARIOBA – Mwenyekiti;
2. Mheshimiwa Jaji Mkuu Mstaafu, Augustino RAMADHANI -Makamu Mwenyekiti;
3. Mheshimiwa Dkt. Salim Ahmed SALIM – Mjumbe;
4. Ndugu Abubakar Mohammed ALI – Mjumbe;
5. Ndugu Ally Abdullah Ally SALEH – Mjumbe;
6. Mheshimiwa Al-Shaymaa J. KWEGYIR (Mb.) – Mjumbe;
7. Ndugu Awadh Ali SAID – Mjumbe;
8. Dkt. Edmund Adrian Sengondo MVUNGI – Mjumbe;
9. Ndugu Esther P. MKWIZU – Mjumbe;
10. Ndugu Fatma Said ALI – Mjumbe;
11. Ndugu Humphrey POLEPOLE – Mjumbe;
12. Ndugu Jesca Sydney MKUCHU – Mjumbe;
13. Ndugu John J. NKOLO – Mjumbe;
14. Ndugu Joseph BUTIKU – Mjumbe;
15. Ndugu Kibibi Mwinyi HASSAN – Mjumbe;
16. Ndugu Maria Malingumu KASHONDA – Mjumbe;
17. Ndugu Muhammed Yussuf MSHAMBA – Mjumbe;
18. Ndugu Mwantumu Jasmine MALALE – Mjumbe;
19. Prof. Mwesiga L. BAREGU – Mjumbe;
20. Ndugu Nassor Khamis MOHAMMED – Mjumbe;
21. Ndugu Omar Sheha MUSSA – Mjumbe;
22. Prof. Palamagamba J. KABUDI – Mjumbe;
23. Mheshimiwa Raya Suleiman HAMAD – Mjumbe;
24. Ndugu Richard Shadrack LYIMO – Mjumbe;
25. Ndugu Riziki Shahari MNGWALI – Mjumbe;
26. Alhaj Said EL- MAAMRY – Mjumbe;
27. Ndugu Salama Kombo AHMED – Mjumbe;
28. Ndugu Salma MAOULIDI – Mjumbe;
29. Ndugu Simai Mohamed SAID – Mjumbe;
30. Ndugu Suleiman Omar ALI – Mjumbe;
31. Ndugu Ussi Khamis HAJI – Mjumbe;
32. Ndugu Yahya MSULWA – Mjumbe;
33. Ndugu Assaa Ahmad RASHID – Katibu; na
34. Ndugu Casmir Sumba KYUKI – Naibu Katibu.
Mheshimiwa Spika,
21. Kwa namna ya pekee, nampongeza Mheshimiwa Jaji Joseph Sinde Warioba, Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais Mstaafu kwa kuteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba na Mheshimiwa Augustino Ramadhani, Jaji Mkuu Mstaafu wa Tanzania kwa kuteuliwa kuwa Makamu Mwenyekiti. Vilevile, napenda kuwapongeza Wajumbe wote, wakiwemo Katibu na Naibu Katibu kwa kuteuliwa kuunda Tume hii. Ni matumaini yangu na ya Watanzania wote kwa ujumla kuwa, Wajumbe wa Tume watatumia ujuzi, maarifa na uzoefu wao katika kuhakikisha wanatekeleza majukumu waliyopewa kwa mujibu wa Sheria na kwa ufanisi mkubwa.
Serikali ilivyojipanga (Maandalizi ya Tume)
Mheshimiwa Spika,
22. Wakati wa hafla ya kuwaapisha Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti, Wajumbe, Katibu na Naibu Katibu wa Tume, Mheshimiwa Rais aliihakikishia Tume kuwa Serikali itaipa kila aina ya ushirikiano ili itekeleze majukumu yake kwa ufanisi. Kwa niaba ya Serikali kupitia Bunge lako Tukufu, naomba kwa mara nyingine tena nikuhakikishie kuwa Serikali imejipanga kwa kuweka mazingira yatakayoiwezesha Tume kutekeleza majukumu yake kama Sheria ya Mabadiliko ya Katiba (Sura ya 83) inavyoelekeza. Hivi sasa, Serikali inakamilisha maandalizi muhimu kuiwezesha Tume kuanza kazi tarehe 1 Mei 2012 kama ilivyopangwa.
Mheshimiwa Spika,
23. Naomba kutumia fursa hii kuwaomba Wananchi wote kuipa Tume ushirikiano wa kutosha ili iweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi. Vilevile, napenda kuwasihi Wananchi wajitokeze kwa wingi katika Mikutano itakayoitishwa na Tume na watoe maoni yao kwa uhuru na utulivu bila vikwazo vyovyote. Lengo la Serikali ni kuhakikisha kuwa Watanzania wote wanashiriki kikamilifu bila ubaguzi wowote katika mchakato huo wa kuandika Katiba Mpya ili Nchi yetu iweze kupata Katiba itakayokidhi mahitaji ya Karne hii na miaka mingi ijayo.
Mheshimiwa Spika,
24. Napenda kusisitiza maagizo ya Mheshimiwa Rais aliyoyatoa siku ya kuwaapisha Wajumbe wa Tume kwamba Mchakato huu wa Mabadiliko ya Katiba siyo mchakato wa kuwepo au kutokuwepo kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni mchakato unaolenga kukubaliana namna bora ya kuendesha Nchi kwa kuzingatia uwepo wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, uwepo wa Haki za Binadamu na Misingi ya Utawala Bora, uwepo wa Mihimili Mitatu ya Dola yaani Bunge, Mahakama na Serikali na namna nzuri ya kuboresha utendaji kazi wa Mihimili hiyo. Ninawaomba Waheshimiwa Wabunge kuwaelimisha Wananchi juu ya kuzingatia mambo haya ya msingi wakati wa kutoa maoni yao.
MIFUKO YA HIFADHI YA JAMII
Mheshimiwa Spika,
25. Waheshimiwa Wabunge watakumbuka kuwa Bunge lako Tukufu lilipitisha Sheria Namba 8 ya Mwaka 2008 ya kuanzisha Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii.Umuhimu wa Hifadhi ya Jamii Nchini unatambuliwa ndani ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Ibara ya 11(1) inayosomeka, nanukuu:
“Mamlaka ya Nchi itaweka utaratibu unaofaa kwa ajili ya kufanikisha utekelezaji wa Haki ya Mtu Kufanya Kazi, Haki ya kujipatia Elimu na Haki ya kupata Msaada kutoka kwa Jamii wakati wa Uzee, Maradhi au hali ya Ulemavu, na katika hali nyinginezo za mtu kuwa hajiwezi.” Mwisho wa kunukuu.
Hivyo, Hifadhi ya Jamii ni nguzo muhimu katika kutekeleza dhana ya Utawala Bora katika Jamii na kuchochea ukuaji wa Uchumi.
Mheshimiwa Spika,
26. Lengo Kuu la kuwa na Mipango ya Hifadhi ya Jamii ni kuondoa Umaskini wakati wa Uzee na kutoa kinga ya Kiuchumi na Kijamii pale panapotokea matukio na majanga mbalimbali yanayosababisha kupungua kwa kipato. Hivi sasa kuna Mifuko Sita ya Hifadhi ya Jamii ambayo inatoa Mafao ya muda mfupi na muda mrefu kulingana na taratibu zilizopo katika Sheria za Mifuko husika. Mifuko hiyo ni Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF); Mfuko wa Pensheni kwa Mashirika ya Umma (PPF); Mfuko wa Pensheni kwa Watumishi wa Umma (PSPF); Mfuko wa Pensheni kwa Watumishi wa Serikali za Mitaa (LAPF); Mfuko wa Akiba kwa Watumishi wa Serikali (EGPF); na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF).
Mheshimiwa Spika,
27. Kwa mujibu wa takwimu zilizopo, ni Asilimia 5.9tu ya nguvu kazi ya Watanzania waliopo katika Sekta rasmi ndiyo wanaopata huduma ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii. Takwimu hizi ni kielelezo tosha kuonesha changamoto inayoikabili Sekta ya Hifadhi ya Jamii katika kuhakikisha Watanzania wengi wanajiunga na kunufaika na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii. Aidha, changamoto hii si kwa Wananchi wanaojishughulisha katika Sekta isiyo rasmi tu bali hata kwa wale waliopo katika Sekta rasmi ambao kwa namna moja au nyingine hawajajiandikisha katika Mifuko ya Hifadhi ya Jamii.
Mheshimiwa Spika,
28. Changamoto nyingine zinazokabili Mifuko hii ya Hifadhi ya Jamii ni pamoja na kupishana sana kwa Mafao kati ya Mfuko mmoja na mwingine japo kiwango cha kuchangia kinalingana yaani Asilimia 20 ya Mshahara wa Mtumishi. Lipo pia tatizo la Pensheni isiyoendana na gharama za maisha, gharama kubwa za uendeshaji wa Mifuko, huduma hafifu kwa Wanachama wa Mifuko, Kukosekana kwa Kanuni za Uwekezaji zinazolingana pamoja na Idadi kubwa ya Wananchi kutoelewa umuhimu wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii.
Mheshimiwa Spika,
29. Katika kukabiliana na baadhi ya changamoto zilizoko kwenye Sekta hii ya Hifadhi ya Jamii, Serikali imechukua hatua mbalimbali. Moja ya hatua hizo ni kuanzisha na kutekeleza Sera ya Taifa ya Hifadhi ya Jamii ya mwaka 2003 ambayo ni Dira ya shughuli zote za Hifadhi ya Jamii hapa Nchini. Vilevile, mwaka 2008 Serikali ilianzisha Mamlaka ya Hifadhi ya Jamii. Jukumu kubwa la Mamlaka hii ni kusimamia Sekta ya Hifadhi ya Jamii ikiwamo Mifuko yote ya Hifadhi ya Jamii Nchini. Ni matumaini yangu kuwa Mamlaka ya Hifadhi ya Jamii itatusaidia kuzifanyia kazi Changamoto nilizozitaja hapo juu na nyingine ili kuhakikisha kuwa Watanzania wengi wanajiunga na kupata Hifadhi ya Jamii.
Mheshimiwa Spika,
30. Ili kuhakikisha kuwa Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii, Serikali ilileta katika Kikao hiki cha Bunge Muswada wa Marekebisho ya Sheria za Mifuko ya Hifadhi ya Jamii. Nichukue fursa hii kulipongeza Bunge lako Tukufu kwa kupitisha Muswada huu. Muswada huo uliopitishwa na Bunge unalenga kuwianisha Sheria za Mifuko na Sheria ya Mamlaka ya Hifadhi ya Jamii. Lengo ni kuipa Mamlaka uwezo zaidi wa kutekeleza majukumu yake; na kuiwezesha Mifuko kutoa huduma bora kwa Wanachama wake. Muswada huu unaiwezesha pia Mifuko kutambua uwezo wa Mamlaka kuleta mageuzi kwenye Sekta kwa kutoa Miongozo mbalimbali.
Mheshimiwa Spika,
33. Nachukua fursa hii kuwakumbusha Waajiri wanaokiuka Sheria kwa kuwachagulia Wafanyakazi wao wapya, Mifuko ya kujiunga nayo kinyume na matakwa ya Wafanyakazi hao waache kufanya hivyo. Kila Mwajiri anatakiwa kuweka mazingira yatakayomwezesha Mfanyakazi kuchagua Mfuko anaoupenda. Mazingira hayo ni pamoja na kuialika Mifuko yote kutoa maelezo kuhusu Mafao na huduma zao na kuwapa fursa Wafanyakazi kufanya maamuzi ya kujiunga na Mfuko waupendao. Ni matumaini yangu kuwa Mamlaka itaweka Kanuni zitakazowezesha Mifuko kuandikisha Wanachama kwa utaratibu unaokubalika na unaomlinda Mwanachama.
34. Kwa upande wa Uwekezaji, Mamlaka imekamilisha tathmini ambayo itawezesha kutengeneza Miongozo kwa Mifuko kuwekeza katika Vitega Uchumi mbalimbali. Vilevile, Mamlaka itaweka mkakati kabambe wa kuelimisha Umma ili Wananchi wengi zaidi waweze kujiunga na Mifuko hii kwa kuwa sasa wanaruhusiwa kujiunga na Mifuko hiyo bila kujali kama wako Sekta Rasmi au isiyo Rasmi. Napenda pia kutumia fursa hii kutoa wito kwa Waheshimiwa Wabunge na Wananchi wote kutoa ushirikiano stahiki kwa Mamlaka ili kwa kushirikiana na Wadau mbalimbali tuboreshe, tuimarishe na kuwa na Sekta ya Hifadhi ya Jamii iliyo endelevu.
MATOKEO YA MTIHANI WA KUMALIZA ELIMU YA MSINGI MWAKA 2011
Mheshimiwa Spika,
35. Mwaka 2011 Wanafunzi 983,545 wa Darasa la Saba walifanya mtihani wa Taifa. Kati yao Wanafunzi 567,567,sawa na Asilimia 58.28 ya waliofanya mtihani walifaulu. Kiwango cha Ufaulu cha mwaka 2011, ikilinganishwa na kile cha mwaka 2010 unaonesha kupanda kwa Asilimia 4.76 kutoka Asilimia53.52 ya mwaka 2010 hadi 58.28 mwaka 2011.
Mheshimiwa Spika,
36. Tathmini inaonesha Ufaulu kimasomo umeongezeka kwa masomo ya Hisabati, Kiingereza na Sayansi.
i) Kiwango cha Ufaulu kwa Somo la Hisabati kilikuwa Asilimia 39.4 mwaka 2011ikilinganishwa na Asilimia 24.7 mwaka 2010;
ii) Kiwango cha Ufaulu kwa Somo la Kiingereza kilikuwa Asilimia 46.7 mwaka 2011ikilinganishwa na Asilimia 36.5 mwaka 2010; na
iii) Kiwango cha Ufaulu kwa Somo la Sayansi kilikuwa Asilimia 61.3 mwaka 2011 ikilinganishwa na Asilimia 56.1 mwaka 2010.
37. Taarifa zinaonesha kuwa kiwango cha ufaulu kwa masomo ya Kiswahili na Maarifa ya Jamii kilishuka kwa mwaka 2011 ikilinganishwa na mwaka 2010. Kwa mfano, Ufaulu kwa Somo la Kiswahili ulikuwa Asilimia 68.6 mwaka 2011 ikilinganishwa na Asilimia 71.0 mwaka 2010; na kiwango cha ufaulu kwa Somo la Maarifa ya Jamii kilikuwa Asilimia 54.8 mwaka 2011 ikilingnishwa na Asilimia 68.0 mwaka 2010.
Mheshimiwa Spika,
38. Ni kweli kwamba, kwa muda mrefu tumekuwa na matatizo ya ufaulu katika masomo ya Sayansi Nchini, lakini matokeo ya mwaka 2011 yanaonesha kuwa juhudi zinazochukuliwa na Serikali katika kukuza masomo hayo zimeanza kuzaa matunda. Napenda kuwapongeza Wanafunzi, Wazazi, Walezi, Walimu na Watendaji wote walioshiriki katika kuleta mafanikio hayo.
Uchaguzi wa Wanafunzi kuingia Kidato cha Kwanza mwaka 2012
Mheshimiwa Spika,
39. Katika Uchaguzi wa kuingia Kidato cha Kwanza mwaka 2012, jumla ya Wanafunzi 515,187, sawa na Asilimia 90.1 ya Wanafunzi waliofaulu walichaguliwa kuingia Kidato cha Kwanza katika Shule za Sekondari za Serikali. Idadi hii iliongezeka kwa Asilimia 12.49 kutoka Wanafunzi 456,350 mwaka 2010. Taarifa nilizopokea kutoka Mikoa 12 ya Arusha, Dar es Salaam, Dodoma, Iringa, Mara, Morogoro, Mwanza, Lindi, Kilimanjaro, Pwani, Ruvuma na Tanga,
zinaonesha kuwa Wanafunzi wote waliofaulu wamejiunga na Kidato cha Kwanza. Nitumie nafasi hii kuipongeza Mikoa hii kwa kuhakikisha kuwa hakuna Wanafuzi waliofaulu na kushindwa kujiunga na Sekondari.
40. Hata hivyo, sehemu kubwa ya Mikoa niliyoitaja inaonesha kuwepo kwa uhaba mkubwa wa Vyumba vya Madarasa na Madawati. Naiagiza Mikoa yote kuhakikisha mapungufu haya yanashughulikiwa katika Bajeti ya mwaka 2012/2013. Aidha, Mikoa iwe na Mipango endelevu ya kujenga Vyumba vya Madarasa na kutengeneza Madawati badala ya kusubiri matokeo ya Mtihani na kuchaguliwa kwa Wanafunzi ndipo ianze kuweka mikakati.
Matokeo ya Kidato cha Nne mwaka 2011
Mheshimiwa Spika,
41. Matokeo ya Kidato cha Nne ya mwaka 2011 yanaonesha kuwa Wanafunzi 181,880, sawa na Asilimia 53.6ya Wanafunzi 339,330 waliofanya Mtihani walifaulu. Kiwango hicho kimeongezeka kutoka Wanafunzi 177,011 waliofaulu mwaka 2010 ikiwa ni sawa na Asilimia 50.4 ya Wanafunzi 351,214 waliofanya Mtihani.
Mheshimiwa Spika,
42. Tangu mwaka 2008, Asilimia ya Wanafunzi wanaofeli Mitihani ya Kidato cha Nne imekuwa ikiongezeka na kufikia Asilimia 16.3,mwaka 2009 Asilimia 27.5, mwaka 2010 Asilimia 49.6 na kushuka tena hadi Asilimia 43.3, mwaka 2011. Sababu za kushuka kwa ufaulu huo ni pamoja na upungufu wa Walimu, Vifaa vya Kufundishia na kujifunzia na kuimarika kwa udhibiti wa uvujaji wa mitihani ya Kidato cha Nne. Vilevile, inaelezwa na Wanataaluma na Watafiti kwamba kuondolewa kwa Mtihani wa Kidato cha Pili kumechangia sana matokeo mabaya ya Kidato cha Nne.
Mheshimiwa Spika,
43. Kutokana na hali ya kuongezeka kwa idadi ya Wanafunzi wanaofeli Mtihani wa Kidato cha Nne, Serikali imechukua hatua kadhaa zikiwemo za kuongeza na kuimarisha usimamizi wa matumizi ya ‘capitation grant’ ili kupunguza tatizo la upungufu wa Vifaa vya Kufundishia na Kujifunzia Shuleni; Kutekeleza mikakati ya kuongeza idadi na ubora wa Walimu; na kujenga uwezo wa Wakuu wa Shule kusimamia ufundishaji na ujifunzaji wa kila siku.
44. Ni matarajio yangu kwamba tukiyafanya haya, tutaweza kufikia Azma yetu ya kuwa na matokeo mazuri katika siku zijazo. Niwaombe Wadau wote wa Elimu wakiwemo Waheshimiwa Wabunge, Viongozi, Walimu, Wazazi, Walezi na Wanafunzi kila mmoja atimize wajibu wake katika utoaji wa Elimu kuanzia, Nyumbani, Shuleni na Vyuoni ili tuweze kuinua Kiwango cha Ubora wa Elimu Nchini.
MAENDELEO YA VIWANDA
Mheshimiwa Spika,
45. Tarehe 16 hadi 23 Septemba 2011 nilifanya ziara Mkoa wa Mara na kutembelea Kiwanda cha Nguo cha Musoma Textile (MUTEX). Tarehe 2 hadi 4 Desemba 2011 nilifanya ziara nyingine fupi Mkoa wa Mwanza na kutembelea Kiwanda cha kutengeneza Nguo cha Mwanza Textile (MWATEX). Kwa kweli nilikuta Viwanda hivyo vinakabiliwa na changamoto nyingi zikiwemo za kukosekana kwa umeme wa uhakika, Wataalam na teknolojia ya kisasa. Nilielezwa kuwa changamoto hizo zinavikabili Viwanda vingi vya Nguo Nchini.
Mheshimiwa Spika,
46. Sote hapa tunafahamu kuwa maendeleo makubwa na ya kasi kwenye Nchi mbalimbali Ulimwenguni yalichangiwa kwa kiasi kikubwa na maendeleo ya Viwanda vya Nguo na Mavazi. Viwanda hivi hutoa Soko la uhakika kwa zao la Pamba linalolimwa hapa Nchini; huajiri kiasi kikubwa cha Wafanyakazi na hivyo kuwa na mchango mkubwa katika kupunguza tatizo la ajira na umaskini hasa miongoni mwa Vijana. Pia, huchangia Mapato kwa Serikali na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii. Kutofanya vizuri kwa Viwanda hivi kunaikosesha Serikali na Wananchi Mapato na kuongeza tatizo la ajira Nchini. Niliona kuna umuhimu wa kutafuta ufumbuzi wa changamoto zilizo ndani ya uwezo wa Serikali.
Mheshimiwa Spika,
47. Tarehe 23 Machi 2012, niliitisha Mkutano wa Wadau wa Sekta Ndogo ya Viwanda vya Mavazi na Nguo ili kwa pamoja tuweze kuainisha changamoto zinazoikabili Sekta hiyo na kupata mapendekezo ya namna ya kukabiliana na changamoto hizo. Kufuatia Mkutano huo, iliundwa Timu ya Wataalam ili iweze kuangalia changamoto hizo kwa kina na kutoa mapendekezo ya hatua za kuchukuliwa na Serikali pamoja na Wadau wote ili kukabiliana na changamoto hizo. Timu hiyo ilipewa mwezi mmoja na wakati wowote kuanzia sasa itawasilisha taarifa yake Serikalini.
Mheshimiwa Spika,
48. Tarehe 15 Aprili 2012, nilipata fursa ya kutembelea viwanda vya Sunflag (Tanzania) Ltd, Kiwanda cha A to Z na Minjingu Mines and Fertilizer Limited vyote vya Mkoani Arusha. Katika Viwanda vya Nguo vya Sunflagna A to Z nilifarijika kuona idadi kubwa ya Watumishi walioajiriwa na kwamba zaidi ya Asilimia 80 walikuwa ni akina Mama. Nawapongeza Viongozi wa Viwanda hivi kwa jitihada ambazo wanazifanya kuendeleza uzalishaji na hivyo kuchangia Mapato kwa Serikali na Ajira kwa Wananchi.
Mheshimiwa Spika,
49. Kiwanda cha Sunflag ni Kiwanda pekee Nchini kinachozalisha nguo kuanzia hatua ya Pamba kutoka kwa Mkulima hadi nguo za kuvaa. Sunflag wamekuwa ni Soko zuri na la uhakika la Pamba ya Wakulima. Nawapongeza kwa uamuzi wao huo ambao una faida kubwa kwa Wakulima wa Pamba. Viongozi wa Viwanda hivyo walinieleza changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo. Serikali itafanya kila lililo ndani ya uwezo wake kuimarisha Viwanda vinavyotumia pamba ya Tanzania na kuweka mazingira yatakayoendelea kuvutia uwekezaji katika Sekta hii ya Nguo na Mavazi. Baada ya kupata taarifa ya Timu niliyoitaja hapo awali, Serikali itachukua hatua zitakazoondoa changamoto zinazovikabili Viwanda vya Nguo na Mavazi Nchini.
Mheshimiwa Spika,
50. Katika Kiwanda cha Minjingu Mines and Fertilizer Limited nilielezwa kuwa wamefanikiwa kuzalisha mbolea ya Minjingu Mazao ambayo ni bora kuliko Mbolea aina ya DAP kwa kuwa ina virutubisho vya Nitrogen, Phosphorous, Sulphur, Calcium na rutuba kama Magnesium, Zinc na Boroni. Aidha, Minjingu Mazao ina bei ndogo kuliko DAP. Kiwanda kwa sasa kina akiba (stock) ya Tani 5,600 ya Phosphate na Tani 7,100 ya Minjingu Mazao. Nilielezwa kuwa matumizi ya Mbolea ya Minjingu Nchini yamekuwa yakipungua mwaka hadi mwaka kutokana na matatizo mbalimbali ikiwemo hujuma inayofanywa kwenye Mfumo wa Ruzuku za Pembejeo. Napenda kuhimiza Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika ione namna ya kukikwamua Kiwanda cha Minjingu kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI ili kuongeza matumizi ya mbolea za Minjingu.
SENSA YA WATU NA MAKAZI YA MWAKA 2012
Mheshimiwa Spika,
51. Itakumbukwa kuwa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati akitoa hotuba yake ya kumaliza mwaka 2011 alitangaza rasmi dhamira ya Serikali kufanya Sensa ya Watu na Makazi ambayo imepangwa kufanyika Nchini kote tarehe 26 Agosti 2012. Mheshimiwa Rais alisisitiza kuwa Sensa ya Watu na Makazi pamoja na Vitambulisho vya Taifa ni mojawapo ya vipaumbele vya Taifa kwa mwaka huu wa 2012. Tarehe 12 Aprili 2012, Waheshimiwa Wabunge walipata fursa ya kuhudhuria Semina kuhusu Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012. Katika Semina hiyo yalitolewa maelezo ya kina kuhusu hatua iliyofikiwa katika maandalizi ya Sensa ya Watu na Makazi. Nina imani kuwa baada ya Semina hiyo ya tarehe 12 Aprili 2012, hivi sasa Waheshimiwa Wabunge wana uelewa mpana kuhusu umuhimu wa taarifa zitokanazo na Sensa na kwamba watatumia uelewa huo kuwaelimisha Wananchi umuhimu wa kujiandikisha.
Mheshimiwa Spika,
52. Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012 madhumuni yake makubwa ni kupata takwimu kuhusiana na idadi ya Watu na kukusanya Taarifa za kina za Kiuchumi, Kijamii na Maelezo ya Makazi. Taarifa hizi hutumiwa na Serikali na Taasisi nyingine kwa shughuli mbalimbali za Mipango na maendeleo. Serikali pia hutumia Takwimu zitokanazo na Sensa katika kutunga Sera, kufanya maamuzi juu ya Utawala wa Umma kwa kuzingatia mahitaji halisi na vigezo vingine kama vile umri, jinsia na vinginevyo.
Mheshiwiwa Spika,
53. Sensa ya mwaka 2012 ina umuhimu wa kipekee kwa kuwa taarifa zitakazokusanywa zitatumika kufuatilia na kutathmini utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo ya Mwaka 2025 kwa Tanzania Bara na mwaka 2020 kwa Tanzania Zanzibar. Vilevile, taarifa hizo zitatumika kutathmini Mkakati wa Kukuza na Kupunguza Umaskini Tanzania Bara (MKUKUTA) na Mkakati wa Kupunguza Umaskini Tanzania Zanzibar (MKUZA). Takwimu hizo zitatumika pia kutathmini utekelezaji wa Malengo ya Milenia ifikapo mwaka 2015; Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano wa 2011/2012 – 2015/2016 pamoja na kubuni mikakati ya utekelezaji wa Mpango Elekezi wa Miaka 15 wa Utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo hadi mwaka 2025.
Mheshimiwa Spika,
54. Pamoja na maandalizi yanayoendelea hivi sasa, mafanikio ya Sensa yatategemea sana ushiriki wa Umma na Wadau wengine. Sisi Waheshimiwa Wabunge ni Wajumbe wa Kamati za Sensa za Wilaya na Halmashauri zetu na moja ya majukumu ya Kamati hizo ni kuhamasisha na kuelimisha Umma kuhusu umuhimu wa Sensa ya Watu na Makazi ili kuhakikisha kuwa kila mtu atakayelala Nchini Usiku wa Kuamkiasiku ya Sensa, yaani tarehe 25 Agosti 2012 kuamkia tarehe 26 Agosti 2012, anahesabiwa, na kwamba anahesabiwa mara moja tu.
Mheshimiwa Spika,
55. Zoezihili ni la Kitaifa hivyo linahitaji uhamasishaji na ushirikishwaji wa Wananchi wote. Natoa wito kwa Wananchi wote kushiriki kikamilifu katika zoezi la Sensa ya Watu na Makazi na kutoa ushirikiano mkubwa kwa Makarani wa Sensa watakaofanya kazi ya Kuhesabu Watu siku ya tarehe 26 Agosti 2012. Vilevile, naomba nitumie fursa hii kuwaomba Waheshimiwa Wabunge washirikiane na Viongozi wengine kusimamia utekelezaji wa shughuli zote za Sensa katika Wilaya na Halmashauri kwa kuhakikisha kuwa elimu kwa Wananchi inatolewa. Nawaomba pia Waheshimiwa Wabunge kutumia nafasi zao kama Wawakilishi wa Wananchi kuhamasisha na kuelimisha Umma kuhusu umuhimu wa kushirikiana na Makarani wa Sensa wakati wa kipindi cha kuhesabu Watu kwa kutoa Takwimu sahihi na hivyo kupata taarifa sahihi kwa ajili ya Mipango endelevu ya maendeleo. Kaulimbiu yetu kila wakati iwe ni Sensa kwa Maendeleo ya Taifa: Jiandae Kuhesabiwa. Napenda kuwatakia mafanikio mema katika kazi hii muhimu kwa Taifa letu.
MPANGO WA KUTOA KIFUTA MACHOZI CHA MIFUGO
Mheshimiwa Spika,
56. Mwaka 2008/2009, Mikoa ya Kaskazini hasa Mikoa ya Arusha na Manyara ilikumbwa na ukame mkubwa ambao ulisababisha Vifo kwa Mifugo. Kutokana na ukubwa wa tatizo hilo, Mheshimiwa Rais aliahidi kutoa Kifuta Machozi kwa
kuwapatia Mifugo ya Mbegu Wafugaji waliopoteza Mifugo yao yote katika Wilaya za Longido, Monduli na Ngorongoro. Katika kutekeleza Ahadi ya Rais, Serikali iliunda Kikosi Kazi ambacho kilibaini kuwepo kwa Vifo vya Ng’ombe 403,839;Mbuzi 211,201 na Kondoo 121,118 katika Wilaya hizo. Vilevile, Kikosi Kazi kilibaini kwamba jumla ya Kaya 6,127katika Wilaya hizo zilipoteza Mifugo kutokana na ukame. Wilaya ya Longido ilikuwa na jumla ya Kaya 2,852;Monduli Kaya 1,484 na Ngorongoro Kaya 1,791 zilizoathirika na ukame ulioambatana na Vifo na Mifugo.
Mheshimiwa Spika,
57. Katika mwaka 2011/2012, Serikali ilitoa Tamko Bungeni kuhusu kutekeleza ahadi ya kutoa Kifuta Machozi kama mbegu (seed stock) kwa Kaya zilizopoteza Mifugo yote ili ziweze kurudi katika hali yao ya awali kama Wafugaji. Aidha, Mradi maalum ulianzishwa kwa ajili ya kununua Mifugo (Ng’ombe na Mbuzi) kwa ajili ya Wilaya husika. Ununuzi wa Mifugo hiyo utafanyika katika ngazi ya Halmashauri za Wilaya kwa kuzingatia Sheria ya Manunuzi Na. 21 ya mwaka 2004.
Mheshimiwa Spika,
58. Kufuatia kuundwa kwa Kamati mbalimbali (Mkoa, Halmashauri, Kata na Vijiji za kusimamia utekelezaji wa Mpango wa Kusambaza Mifugo ya Kifuta Machozi, Halmashauri za Wilaya zilielekezwa kutangaza zabuni za kuwapata wanunuzi wa Mifugo ndani ya maeneo ya Wilaya husika katika kipindi cha Siku Tisini (90). Utekelezaji wa Zoezi hili utafanyika kwa Awamu kulingana na upatikanaji wa fedha. Aidha, Awamu ya Kwanza itaanza kwa kununua Ng’ombe 500 kwa kila Wilaya. Lengo ni kukamilisha zoezi hili kabla ya Kiangazi kuanza.
Mheshimiwa Spika,
59. Napenda kulijulisha Bunge lako Tukufu kuwa Uzinduzi wa Mpango wa kutoa Kifuta Machozi ulifanywa na Mheshimiwa Rais, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete tarehe 19 Februari 2012 katika Wilaya ya Longido ambapo Serikali ilitumia Shilingi Milioni 213 kwa kununua na kusambaza Ng’ombe 500.
60. Aidha, ununuzi wa Mifugo kwa ajili ya Wilaya za Monduli na Ngorongoro utakamilika mara Serikali itakapokamilisha taratibu za kutuma fedha kwa Halmashauri za Wilaya hizo. Kiasi cha Shilingi Milioni 206 zimetengwa kwa ajili ya Wilaya ya Monduli na Shilingi Milioni 218 kwa ajili ya Wilaya ya Ngorongoro ili kuwezesha ununuzi wa Ng’ombe 500 kwa kila Wilaya.
61. Matumaini yangu ni kuwa zoezi la kutoa Kifuta Machozi kwa Wananchi wa Wilaya za Monduli na Ngorongoro litakamilika katika muda mfupi ujao kwa kuwa Mifugo hiyo ipo tayari kwa Wazabuni. Kinachosubiriwa ni malipo ya fedha. Natoa wito kwa Wafugaji na Wananchi walioathirika na ukame ambao wanasubiri Awamu ya Pili kuwa na subira wakati Serikali inatafuta fedha za kutekeleza Mpango huu.
HITIMISHO
Mheshimiwa Spika,
62. Kabla ya kuhitimisha hotuba yangu, napenda kusisitiza maeneo muhimu yafuatayo:
Kwanza: Tumeanza Mchakato wa Utekelezaji wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba. Mchakato ambao ni Msingi wa Utawala Bora. Natoa wito kwamba, Tuwaelimishe Wananchi kuhusu Mambo ya Msingi wakati wa kuchangia Maoni, na kwamba Mabadiliko ya Katiba siyo Mchakato wa kuwepo au kutokuwepo kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Pili: Tunayo Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ambayo tukiitumia vizuri, ni kinga na kichocheo muhimu cha Kuondoa Umaskini na Kukuza Uchumi. Tushirikiane na Mamlaka ya Hifadhi ya Jamii kuwaelimisha Wananchi kuhusu umuhimu wa kujiunga na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kwa faida yao, kwani hivi sasa haijalishi kama uko kwenye Sekta Rasmi au Isiyo Rasmi.
Tatu: Bado tunazo changamoto nyingi katika Sekta ya Elimu, hasa katika Miundombinu na Ubora wa Elimu kwa ujumla. Tushirikiane katika kutekeleza Mikakati ya kutuwezesha kuwa na Elimu Bora kwa Watoto wetu. Tuwajengee utamaduni wa kujiamini na kushiriki kikamilifu katika kuboresha Miundombinu muhimu kuanzia Shule za Msingi, Sekondari hadi Vyuo.
Nne: Kuwepo kwa Viwanda Nchini ni muhimu kwa maendeleo yetu na Uchumi wa Nchi. Pamoja na changamoto zilizopo ni vizuri kuweka umuhimu wa kutumia bidhaa zinazozalishwa na Viwanda vyetu.
Tano: Tarehe 26 Agosti 2012 itakuwa ni Siku ya Sensa ya Watu na Makazi Nchini. Tuwahamasishe Wananchi waelewe umuhimu wa kuhesabiwa siku hiyo na utaratibu utakaotumika ikiwa ni pamoja na kila Mtu kuhakikisha anahesabiwa na kwamba anahesabiwa mara moja tu.
Mheshimiwa Spika,
63. Tunapohitimisha Mkutano huu wa Saba, pamoja na kumshukuru Mwenyezi Mungu tunao wajibu wa kiungwana kuwashukuru pia wote walioshiriki katika kutoa huduma muhimu katika kufanikisha Mkutano huu. Nitumie fursa hii kutoa shukrani za dhati kwako wewe Mheshimiwa Spika kwa kutuongoza vizuri na hatimaye kukamilisha Vikao vyote kama ilivyopangwa. Vilevile, namshukuru Naibu Spika pamoja na Wenyeviti wa Bunge kwa kazi nzuri. Niruhusu nimshukuru Dkt. Thomas Kashilillah, Katibu wa Bunge na Wasaidizi wake kwa kutuwezesha kufanya kazi hii kwa ufanisi mkubwa. Niwashukuru pia Wataalam wote ambao mchango wao kwetu umekuwa ni muhimu sana. Niwashukuru Askari, Madereva, Wanahabari kwa kushiriki kikamilifu katika kufanikisha Mkutano huu.
Mheshimiwa Spika,
64. Leo tunapohitimisha Mkutano huu wa Saba, tunapata fursa ya kujiandaa kwa ajili ya Mkutano wa Nane ambao ni Mahsusi kwa ajili ya Bajeti ya Mwaka 2012/2013. Napenda kuwatakia maandalizi mema kwa ajili ya Bajeti ya Serikali. Ni dhahiri kwamba bado tuna changamoto nyingi. Nawasihi kila mmoja wetu kujiwekea malengo ya kutimiza wajibu wake katika kufikia yale yote tunayoyatarajia kuyafanya kwa ajili ya Maendeleo ya Nchi yetu. Nimalizie kwa kuwatakia nyote safari njema ya kurejea katika maeneo yenu ya kazi.
Mheshimiwa Spika,
65. Baada ya kusema haya, naomba kutoa hoja kwamba Bunge lako Tukufu liahirishwe hadi tarehe 12 Juni 2012 Saa 3:00 Asubuhi, litakapokutana kwenye Ukumbi huu hapa Mjini Dodoma kujadili Bajeti ya Serikali.
66. Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.
No comments:
Post a Comment